ACT Wazalendo yashinda Jimbo la Konde kwa asilimia 72

NA GODFREY NNKO

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Konde kisiwani Pemba, Mohamed Said Issa kupitia Chama cha ACT Wazalendo ametangazwa mshindi katika uchaguzi mdogo wa jimbo hilo kwa kupata kura 2391 sawa na asilimia 72.
Katika uchaguzi huo mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mbarouk Amour Habib amepata kura 794 akifuatiwa na Salama Khamis Omar wa Chama cha Wananchi (CUF) aliyepata kura 98 na Hamad Khamis Mbarouk wa Chama cha AAFP aliyepata kura 55 kati ya kura 3,338 zilizopigwa.

Msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Konde, Abdallah Said Ahmed amemtangaza Mohamed Said Issa leo Jumamosi Oktoba 9, 2021 katika kituo cha majumuisho cha Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.

ACT WAZALENDO wanpata ushindi huu baada ya Mbunge mteule wa Jimbo la Konde, Sheha Mpemba Faki kujiuzulu nafasi hiyo kwa kile kilichoelezwa kuwa ni changamoto za kifamilia, jambo ambalo lilipokelewa na chama chake cha CCM.
Faki (pichani) alichaguliwa katika uchaguzi mdogo uliofanyika Julai 18, mwaka huu ambapo CCM ilishinda katika jimbo hilo pamoja na kata sita zilizoshiriki uchaguzi huo ambapo ilishinda bila kupingwa katika kata nne miongoni mwa hizo.

Alijiuzulu kabla hajaapishwa na Spika wa Bunge zikiwa zimepita siku 14 tu tangu alipochaguliwa katika uchaguzi uliohusisha pia chama cha ACT-Wazalendo ambacho kilipoteza jimbo hilo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Agosti 2, mwaka huu na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, Faki aliandika barua ya kujiuzulu ambapo alieleza kufikia uamuzi huo kutokana na changamoto za kifamilia.

“Chama Cha Mapinduzi kimepokea kwa masikitiko makubwa barua ya kujiuzulu kwa mbunge wa mteule wa CCM jimbo la Konde, Sheha Mpemba Faki leo Agosti 2, 2021,” alisema Shaka katika taarifa yake.

Shaka alisema, chama hakina uwezo wa kumzuia katika uamuzi wake huo hasa ikizingatiwa ni haki yake ya msingi kama ilivyo kwa haki ya kuomba ridhaa ya kugombea nafasi ndani ya CCM.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news