NA MWANDISHI MAALUM
Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe amefika katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda Maalum ya Dar es Salaam leo kwa ajili ya kusubiri hukumu dhidi ya Cyprian Musiba.
Hukumu hiyo ni ya shauri la kesi namba 220 ya mwaka 2018 ambapo kesi hiyo iliitwa kwa mara ya kwanza Februari 26, 2019.
Katika kesi hiyo Membe amemshtaki Musiba, Mhariri wa gazeti la Tanzanite na Wachapishaji wa gazeti hilo ambapo anawadai Tsh. Bilioni 10 kwa kumchafua, hukumu hiyo inatarajiwa kutolewa mbele ya Jaji Joacquine De Melo.
Musiba katika kesi hiyo anashtakiwa kwa kumtuhumu Membe kuwa anamhujumu Rais John Magufuli asitekeleze majukumu yake ya kuwaletea wananchi maendeleo huku akidai kwamba mbinu mojawapo ya kukamilisha hujuma hizo ni maandalizi anayofanya kugombea urais mwaka 2020 kupitia CCM.
Mheshimiwa Bernard Membe alikuwa miongoni mwa wagombea Urais katika Uchaguzi Mkuu 2015.