NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Cyprian Musiba ameamuriwa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kumlipa fidia ya Shilingi bilioni Sita aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje katika Serikali ya Awamu ya Nne, Mheshimiwa Bernard Membe.
Hukumu hiyo kwa mwanahabari huyo anayejitambulisha kama mwanaharakati huru imetolewa leo Oktoba 28,2021 na Jaji Joacquine De Mello aliyeisikiliza kesi hiyo.
Wakati huo huo, Mahakama imeweka zuio la kudumu kwa Cyprian Musiba la kutokumkashifu Mheshimiwa Membe au kusema uongo dhidi yake.
Katika hukumu hiyo Musiba ametakiwa kumlipa Membe kiasi hicho cha fedha pamoja na gharama zote za uendeshaji wa kesi kwa zaidi ya miaka miwili.
Hukumu hiyo ni ya shauri la kesi namba 220 ya mwaka 2018.
Mahakama imesema Shilingi Bilioni 5 ni fidia ya hasara halisi na Shilingi Bilioni 1 hasara ya jumla.
Katika kesi hiyo, Mheshimiwa Membe alimshtaki Musiba, Mhariri wa Gazeti la Tanzanite na wachapishaji wa gazeti hilo ambapo aliwadai Shilingi Bilioni 10 kwa kumchafua.
Musiba katika kesi hiyo alishtakiwa kwa kumtuhumu Mheshimiwa Membe kuwa anamhujumu Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli asitekeleze majukumu yake ya kuwaletea wananchi maendeleo, huku akidai kwamba mbinu mojawapo ya kukamilisha hujuma hizo ni maandalizi anayofanya kugombea urais mwaka 2020 kupitia CCM.