DKT.BITEKO AWATAKA GST KUTOA SEMINA KWA WACHIMBAJI WADOGO

Na Steven Nyamiti, WM

WAZIRI wa Madini, Dkt. Doto Biteko ameitaka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kutoa semina kwa wachimbaji wadogo waliopo Mkoa wa Mwanza kuhusu mbinu za utafiti wa madini na namna bora ya kufanya uchenjuaji wa madini ili waweze kuongeza uzalishaji katika shughuli zao.
Dkt.Biteko ametoa agizo hilo leo Oktoba 11, 2021 alipokutana na kusikiliza changamoto za wachimbaji, wafanyabiasha pamoja na viongozi wa wachimbaji madini katika ziara yake aliyoifanya mkoani Mwanza

Akijibu hoja ya Mbunge wa Jimbo la Sengerema, Khamis Tabasamu aliyewasilisha ombi ili STAMICO iende kusaidia shughuli za uchorongaji katika Wilaya ya Kwimba, Waziri Dkt. Biteko amemuagiza Kaimu Mkurugenzi wa STAMICO, Dkt.Venance Mwase kukamilisha utaratibu ili waende Kwimba wakafanye uchorongaji kama inavyofanyika mahali kwingine.
Wakati huo huo akizungumzia migogoro ya ardhi inayotokea kwa wachimbaji wa madini kuhusu umiliki wa ardhi, Dkt.Biteko amesema, haki ya madini na ardhi ni haki sawa zinazosimamiwa na Sheria ya Madini na Sheria ya Ardhi huku akisisitiza hakuna mwenye sheria ya juu kuliko mwenzake.

’’Hakuna mwenye ardhi, ardhi hii ni mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hakuna mwenye madini, madini haya ni mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,’’amesisitiza Dkt. Biteko.

Pia, Dkt.Biteko ameeleza kuwa, Serikali inakamilisha utaratibu wa kusajili viwanda vya kusafisha Dhahabu (Refinery) vilivyopo Mwanza, Geita na Dodoma.

Waziri Dkt.Biteko amesema, hadi sasa kuna viwanda vitatu vya kusafisha dhahabu vitakavyotumika kusafisha dhahabu kabla ya kusafirishwa nje ya nchi ili kuongeza thamani ya madini kabla ya kusafirishwa.

Aidha, Dkt.Biteko amefafanua kuwa, mpango wa Serikali ni kuona watanzania katika shughuli za uchimbaji madini wanafanya kazi zao kwa uhuru bila kuonewa, kunyanyaswa huku wakilipa kodi stahiki kwa maendeleo ya nchi.

Katika hatua nyingine, Dkt.Biteko amewataka Wafanyabiashara wa madini Mkoa wa Mwanza wenye ofisi katika jengo la Rock City Mall kuhamia katika soko jipya la madini lililopo katika eneo la Kiwanda cha Kusafisha Dhahabu cha Mwanza Precious Metals Limited.
Naye Naibu Waziri wa Ardhi, Dkt.Angelina Mabula amesema, kuanzishwa kwa kiwanda cha kisasa cha kusafisha dhahabu cha Mwanza Precious Metals kimesaidia kutoa ajira na kitakuza uchumi kwa wanachi wa Ilemela na Mwanza kwa ujumla.

Amesema, lengo la Serikali ni kuhakikisha inaondoa changamoto za wachimbaji wa kuanzisha kituo cha pamoja katika kiwanda hicho ili kutoa huduma zote kwa urahisi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Mwanza (MWAREMA), Richard Seni amesema kuwa, wachimbaji wadogo wameendelea kushiriki katika utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii.

Aidha, amemuomba Waziri Dkt.Biteko kuzungumza na Sekta za Kibenki ili zikopeshe wachimbaji wadogo na wapate kinga ya kupata mikopo kwa shughuli mbalimbali za madini.

Mfanyabiashara wa Madini akiwasilisha hoja kwa Waziri wa Madini, Dkt.Doto Biteko (hayupo pichani) wakati wa kikao cha wafanyabiashara na wachimbaji mkoani Mwanza. (Picha zote na Steven Nyamiti-WM).

Kikao cha Waziri wa Madini, Dkt.Biteko kimehudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, Mbunge wa Jimbo la Sengerema, Khamisi Tabasamu, Kaimu Mkurugenzi wa STAMICO, Dkt. Venance Mwase, Kamishina Msaidizi Francis Mihayo, Mkurugenzi wa Biashara na Ukaguzi wa Madini Tume ya Madini Venance Kasiki, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mwanza, Ernest Maganga, pamoja na wachimbaji, wafanyabiashara na viongozi wa wachimbaji wa madini wa Mkoa wa Mwanza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news