DPP aombwa kufuta kesi ya Mbowe,Mungai asema mtaani bado wapo kina Sabaya

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Leo Oktoba 18, 2021 wenyeviti wa mikoa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wamemtembelea Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe katika gereza la Ukonga lililopo katika Halmashauri ya Jiji la Ilala, Dar es Salaam ili kumjulia hali na kumtia moyo katika kesi inayomkabili.

Mheshimiwa Mbowe anayekabiliwa na kesi ya ugaidi leo ametimiza siku 90, tangu alipokamatwa jijini Mwanza ambako alikuwa akiongoza kikao cha kuhamasisha kupatikana kwa katiba mpya.
William Mungai ambaye ni Mwenyekiti wa msafara huo na pia Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Mkoa wa Iringa, amesema wamefurahi kwa kuwa, wamekuta Mheshimiwa Freeman Mbowe ana afya njema na yuko imara katika mapambano.

"Tumemuona Mwenyekiti wetu yuko imara na ametuhakikishia kwamba afya yake ni njema katika mazingira aliyopo. Yupo anajisomea vitabu, tunaamini akitoka atakuwa bora zaidi,"amesema Mungai.

Hata hivyo, amewataka wananchi waendelee kufuatilia kesi ya Mbowe ambayo itaendelea Oktoba 20, mwaka huu.

"Siasa ni uchumi, ukitaka uchumi ukue weka siasa safi, ukitaka jamii iendelee lazima kuwe na siasa safi na sasa tunamuomba DPP afute kesi inayomkabili Freeman Mbowe, kwani si gaidi. Amegombea nafasi za urais, ubunge leo unasemaje gaidi,"amesema.

Katika hatua nyingine, William Mungai amesema kuwa, mtaani wapo akina Ole Sabaya wengi ambao wanazunguka mitaani.

"Hivyo tunaomba hao wengine waliobaki wachukuliwe hatua. Wananchi jitokezeni kuwataja na kutoa vithibitisho kwa vyombo viwachukulie hatua. Kina Sabaya hawapaswi kuwa huru mtaani. Ili mambo haya yasijirudie wateule kama DC na RC wasiteuliwe moja kwa moja na Rais, wapitie bungeni kuthibitishwa au wananchi wawachague kwa kura za siri ili kuwa na viongozi wenye kuwatumikia wananchi si kama hivi tunavyoona haya yanayotendeka kama haya ya Sabaya,"amesema Mwenyekiti huyo wa CHADEMA Mkoa wa Iringa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news