NA FRESHA KINASA
SHIRIKA la Hope for Girls and Women in Tanzania linalojishughulisha na mapambano ya Ukatili wa Kijinsia mkoani Mara, limeadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike kwa kutoa elimu ya madhara ya ukatili wa kijinsia na kugawa taulo za kike kwa wanafunzi wanaoishi mazingira magumu wanaosoma katika Shule ya Sekondari Buhemba na Mirwa zilizopo Wilaya ya Butiama.
Afisa Miradi kutoka Shirika
la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT), Debora Boniphace amesema
kuwa lengo la kugawa taulo katika shule hizo ni kuwawezesha
wanafunzi wa kike kumudu kuhudhuria masomo yao, kwani baadhi yao
hushindwa kuhudhuria shule wanapokuwa hedhi na kupelekea kukosa baadhi
ya vipindi, huku elimu ya Ukatili wa Kijinsia akisema itawasaidia
kutambua madhara na kuchukua hatua ikiwemo kuwaelimisha wengine na
jamii.
Ameongeza kuwa, kwa kutambua umuhimu na thamani kubwa ya
elimu kwa watoto wa kike shirika hilo limeamua kufanya hivyo ili
kuunga mkono ufanisi wao wa kitaaluma katika kuwaandaa waje kuwa na
faida kwa jamii na taifa kwa siku za usoni kupitia elimu kwani wataleta mapinduzi chanya katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kwa
upande wake Afisa Mwelimishaji Jamii Madhara ya Ukatili wa Kijinsia
kutoka Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, Emmanuel Goodluck amewataka wanafunzi hao kujitambua na kusoma kwa bidii kusudi
wafikie ndoto zao, ambapo pia amewahimiza kuwa mabalozi wa kutoa elimu
kwa jamii kuhusu madhara ya Ukatili wa Kijinsia ikiwemo ndoa za utotoni,
ukeketaji kwani vitendo hivyo vinamadhara makubwa kwa Ustawi wao wa
kitaaluma na kiafya pia.
"Tambueni kwamba ninyi ni viongozi
katika jamii na katika taifa letu, someni kwa bidii mnapokuwa shuleni
kusudi ndoto zenu zitimie. Elimisheni madhara ya ukatili bila kuogopa
ili elimu iwafikie wanajamii, achaneni na vishawishi ambavyo vitawafanya
mkatishe masomo yenu watoto wa kike mnamchango mkubwa katika maendeleo
kuanzia ngazi ya familia, Jamii hadi taifa,"amesema Goodluck.
Aidha,
Goodluck ameiomba jamii kuwa mstari wa mbele katika kutatua
changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa kikwazo kwa watoto wa kike kufikia
malengo yao, amesema kila mmoja anapaswa kuwajibika kikamilifu
kuhakikisha kwamba wanafikia hatua njema. Na iwapo kuna watu
wanaobainika kuwakwamisha kwa manufaa yao lazima wafichuliwe na
wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Emmanuel Goodluck ambaye ni Afisa Mwelimishaji Jamii Madhara ya Ukatili wa Kijinsia kutoka Shirika la HGWT akizungumza na Wanafunzi wa Mirwa Sekondari wakati wa maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Kike Duniani.
Naye Kaimu Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Butiama, Amani Malima ameiomba jamii kuwapa fursa sawa ya elimu watoto wa kike na wa kiume, huku akiomba watoto wa kike wapunguziwe majukumu wanaporejea nyumbani baada ya masomo kusudi wapate muda mwingi wa kujisomea kama ilivyo kwa watoto wa kiume sambamba na kufuatilia maendeleo yao ya kitaaluma shuleni.
Martha Joseph ni mwanafunzi wa kidato cha tatu Mirwa Sekondari ambapo amelishukuru Shirika la HGWT kwa kugawa taulo za kike kwa wanafunzi wanaoishi mazingira magumu pamoja na kutoa elimu kuhusiana na madhara ya Ukatili wa Kijinsia, ambapo amesema hatua hiyo itachagiza ufauru wao hususan kwa Watoto wa kike kuhudhuria shuleni wakati wa hedhi.
Mathias Peter ni mkazi wa Kata ya Buhemba ambapo amelipongeza Shirika la HGWT kwa namna ambavyo limekuwa likishiriki kupambana na ukatili wa kijinsia kwa njia mbalimbali ikiwemo kutoa elimu katika mikutano ya hadhara, kutumia michezo na kuonesha sinema, hatua ambayo amesema inawafanya wananchi wengi kutambua madhara ya vitendo hivyo. Huku akiomba Jamii kuunga mkono juhudi hizo na serikali.
Tags
Habari