NA HADIJA BAGASHA
HALMASHAURI ya Jiji la Tanga imeahidi kutekeleza agizo la Serikali Kuu la uwazi katika kutoa taarifa za mapato na matumizi na kuweka hadharani mapokezi ya fedha yote kutoka Serikali Kuu kwa kipindi husika.
Alisema, ni takwa la serikali kuona kwamba fedha zote zinazoingia na kutoka ni lazima zitolewe taarifa kupitia vyombo vya habari pamoja na kuzitangaza kupitia mbao za matangazo ili wananchi wazione na kusoma.
“Tukipokea fedha zozote ni lazima wananchi wote wazisome, hali kadhalika wananchi wote wawe na haki ya kufahamu fedha zilizopokelewa zinafanyia kazi gani. Kwa mfano, bweni au darasa linapojengwa, wananchi wanastahili kufahamu gharama na hata mapato yetu yanayokusanywa, yapaswa yafahamike pia,”amesema.
Kauli hiyo ya Mkurugenzi wa Jiji ilikuwa inaunga mkono nasaha za Mtahiki Meya, Abdrahaman Shiloo aliyesisitiza uwazi katika mapokezi na matumizi ya fedha ya serikali, iwe ya makusanyo ya ndani au kutoka serikali kuu.
Hata hivyo pamoja na majadiliano kuhusu miradi ya maendeleo, wajumbe pia walizungumzia kuhusu ukiukwaji wa masharti ya ujenzi uliofanywa na kiwanda cha Rhino kujenga hosteli kiwandani hapo kinyume na masharti ya ujenzi kwani eneo hilo ni kwa shughuli za viwanda tu (industrial area) na sio sehemu ya makazi, na hivyo kuagiza idara husika kufuatilia na kuchukua hatua stahiki ili kurekebisha mapungufu hayo.