NA MWANDISHI MAALUM, Tegeta
'Asiyefanyakazi na asile', huu ni msemo ambao umekuwa ukitajwa sana, hasa katika dini mbalimbali ukihimiza kwamba Mungu amemtaka kila binadamu kufanya kazi ndipo apate riziki au mahitaji yake.
Lakini, pamoja na himizo hili pia zipo baadhi ya dini ambazo bado kwa kutojua au kwa makusudi zimekuwa zikiwafundisha wafuasi wake kwamba kupata riziki au mahitaji ni kwa njia ya Maombi na Miujiza, kwa kuamini kuwa ukiomba utapewa.
Kiongozi Mkuu wa Kanisa Halisi la Mungu Baba, Baba Halisi wa Uzao
Kwamba, maombi pekee yanaweza kumfanya mtu kupata chakula, mavazi, malazi na mahitaji mengine yoyote anayohitaji mwanadamu ikiwemo kupata mume au mke.
Wakati baadhi wakiendelea kuamini katika miujiza na kuzidi kutumbukia katika ufukara, zipo baadhi ya dini au madhehebu yamefunuliwa kuelewa kuwa hakuna kutumaini maombi au miujiza ili binadamu apate riziki au mahitaji yake yoyote bali njia pekee ni kufanya kazi kwa juhudi na maarifa huku ukimtanguliza Mungu mbele kwa ajili ya shukurani kwake unapopata.
Kanisa Halisi la Mungu Baba lililopo Tegeta jijini Dar es Salaam, ni miongoni mwa makanisa pengine machache ambalo linaamini kuwa maombi au miujiza siyo njia ya binadamu kuweza kupata mahitaji ya uhakika ya kila kitu, bali kufanya kazi au uzalaishaji ndiyo njia halisi ambayo inaweza kumfanya binadamu kupata takwa lake.
Kutokana na kuamini hivyo, Kanisa Halisi la Mungu Baba lenyewe linahimiza waumimi wake kuzalisha kwa kuwapa kauli mbiu katika kila ibada kwamba "Ibada ni uzalishaji, Uzalishaji siyo aibu".
Ili kuhamasisha waumini wake kufanya kazi za uzalishaji, Kanisa Halisi la Mungu Baba limekuwa mara kwa mara likifanya Ibada maalumu inayohusiana na dhana hiyo.
Katika mwendelezo wa dhana hiyo, Kanisa hilo limeandaa Ibada Maalum ya Mauzo na Uzalishaji, ambayo itafanyika kwenye Kanisa hilo leo Jumapili, Oktoba 10, 2021 taraehe ambayo kwa kalenda ya Kanisa hilo ni (26 Abu Vol.2), ambapo wanakaribishwa bila ubaguzi wa aina yoyote Wazalishaji na Wafanyabiashara wa bidhaa mbalimbali kwa ajili ya kuuza na kutangaza bidhaa zao.
Katika kuhamasisha wananchi wengi kuhudhuria Ibada hiyo ya kipekee Kiongozi Mkuu wa Kanisa Halisi la Mungu Baba anayetambuliwa kwa jina la Baba Halisi wa Uzao, ametoa maelezo muhimu kufafanua zaidi kwa nini Kanisa linafanya Ibada za uzalishaji,
Ameeleza kuwa, kuanzia lango (siku) Kanisa Halisi la Mungu Baba lilipoanza kufundisha kuwa Ibada ni Uzalishaji, kulitokea maswali ndani na nje ya Kanisa! Walioko ndani ya Kanisa walikutana na kile alichofanya Yesu alipoingia ndani ya Hekalu akakuta Meza za wafanyabiashara na kuzipiga mateke huku akisema nyumba ya Baba yake ni ya sala (Mathayo 21:12-13).
Hawakujua kuwa Yesu alikuwa na maana ya kufukuza wapangaji wabaya ndani ya Moyo, ambao wanatakiwa kufutika ili Mzalishaji azalishe utajiri kwa amani, wapangaji hao ni wale walioandikwa katika Marko7:21-23.
Walioko nje ya Kanisa wao waliona ni mafundisho yasiyoeleweka kwa kuwa walifundishwa kuwa Kanisani ni mahali pa kwenda kumlilia MUNGU wakati wa shida na tabu peke yake.
Hawakukumbuka kuwa, wakati wa kuumba kwa mara ya kwanza, MUNGU BABA yaani CHANZO CHA MEMA NA MAZURI, alianza kwa kuweka HESHIMA na UTAJIRI ndani ya ule Moyo wa Mwanzo aliouengua kushoto kwake (Mithali 3:16).
Aidha, hawakukumbuka kuwa Adamu akiwa bado kwenye kitanga cha Mkono wa CHANZO CHA MEMA NA MAZURI, aliambiwa azalishe, atiishe, aongezeke na amiliki kila kilichoumbwa (Mwanzo 1:28).
Katika yote aliyoambiwa hapo juu la kwanza aliloambiwa Adamu ni kuzalisha.
Baada ya Adamu kutoka kwenye kitanga cha Mkono wa MUUMBA WA VYOTE, WOTE NA YOTE na kuonekana wazi, aliambiwa pia azalishe kwa maana ya kulima na kutunza Bustani ya Edeni (Mwanzo 2:7-15).
Kulima na kutunza Bustani ina maana kazi yoyote ya halali unayoifanya ni kulima na kutunza.
Hiyo ndiyo ibada ambayo CHANZO HALISI aliitaka tangu anaanza kuumba hadi sasa. Waliobadilisha kusudi hilo la CHANZO CHA MEMA NA MAZURI, ni Watumishi ambao walipewa kusimamia shamba lake (Mathayo 21:33-40).
KUSUDI LA ALIYEUMBA VYOTE, WOTE NA YOTE NI LIPI?
Hekima ya yeyote ni jinsi anavyoanza na anavyomaliza kila anachokifanya.Tumeona katika ufunguo kuwa mahali CHANZO CHA MEMA NA MAZURI alipoanzia wakati wa kumuumba Mtu ni kuzalisha (Mwanzo 1:28).
Mahali alipomalizia wakati wa kumuumba Adamu ni kwenye uzalishaji (Mwanzo2:15).
Ukiuliza Wanatheolojia wote, wanakubali kuwa anachotaka MUUMBA WA VYOTE, WOTE NA YOTE ni kuabudiwa na kila alichoumba.
Hata wakati anayenjua Moyo wake wa Mwanzo upande wa kushoto ili aumbe Mbingu na Nchi (Mwanzo 1:1), alitaka kile alichokisikia katika Moyo wake(Zaburi 98), kitokeze ili kumuabudu kwa uhalisia na kweli (Yohana 4:23).
Hivyo,alichoanza nacho kwa Adamu akiwa bado kwenye Kitanga cha Mkono wake na kukisisitiza baada ya kumuumba Adamu, hiyo ndiyo ibada anayoitaka kwa kila aliyeumbwa, yaani Uzalishaji.
Ndiyo maana kwenye Moyo wa Mwanzo baada ya kuuengua kushoto kwake, aliweka heshima na utajiri(Mithali 3:16).
Kuna mifano mbalimbali ya Ibada ni uzalishaji katika kitabu: Nuhukatika Mwanzo 7:1, tunasoma kuwaalikuwa mwenye haki.
Ili ujue kuwa Ibada ni Uzalishaji, Nuhu alitoa ibada kwa CHANZO CHA MEMA NA MAZURI akiwa akiwa anatengeneza Meli au Safina. Ibrahimiambaye alipewa kibali cha kuwa Baba wa Mataifa yote kwa vizazi vinne (Mwanzo 15:16), nayealitoa ibada kupitia Uzalishaji wa mifugo, madini na dhahabu (Mwanzo 13:2).
Katika Mwanzo 26:12-25, tunasoma habari za Isaka kuwa naye pia alitoa Ibada kwa CHANZO HALISI kupitia Uzalishaji Shambani.
Yakobo ambaye naye alikuwa mwenye haki, alitoa Ibada kwa Barabara ya Uzalishaji kwa mujibu wa Mwanzo 30:37-43.
Kana kwamba hiyo haitoshi, Yusufuambaye alikuwa Waziri Mkuu wa Misri,naye alitoa ibada kwa CHANZO HALISI kupitia uzalishaji kwa mujibu wa Mwanzo 41:41-45.
Baada ya kitabu cha Mwanzo kuisha, wakati wa Wana wa Israeli walipokuwa wanatoka Misri kwenda Kaanani, ndipo Musa alipolazimika kuwa na Hema ya Kukutania ili ajue wale anaowaongoza njiani wameshindaje?
Kwa kuwa walikuwa wanakuja na Matunda (Sadaka) kwa Musa, Mitume na Manabii waliofuata baada ya Musa walipenda hiyo barabara ya kutoa Ibada kwa kukusanyikia Hemani.
Pamoja na hayo Kusudi la CHANZO CHA MEMA NA MAZURI halikubadilika, maana hadi sasa bado Ibada ni Uzalishaji.
Katika Kipindi hiki, kitu cha kurekebisha ni hiki;waumini na wafuasi wa Dini na Madhehebu mbalimbali wakijenga shule, vituo vya kuwekea nishati, na ofisi za makampuni yao huwa wanajenga na hema ya kukutania hapo ofisini!.
Kwa kufanya hivyo wanaamini kuwa kutoa Ibada ni lazima uingie kwenye hema ya kukutania ndipo CHANZO HALISI akusikie na kupokea ibada. Kumbe ibada inayotakiwa ni wewe kufanya kazi ambayo ni halali.
Kama Mwalimu anafundisha kwa upendo watoto wakafaulu, hiyo ni Ibada. Daktari au Muuguzi anayefanya kazi yake kwa upendo, hiyo ni Ibada.
Mwanafunzi anayesoma kwa Upendo na utii, hiyo ni ibada.
Dereva anayeendesha boda boda, daladala, basi la abiria kwenda mkoani au lori la bidhaa kwa haki, hiyo ni ibada anayoitaka CHANZO HALISI.
Mfanyabiashara asiyelegeza mizani wakati wa kupima sukari na unga wa ngano dukani, hiyo ni ibada ikiwa na maana ya harufu ya manukato kwa CHANZO HALISI.
Kuhani anayehifadhi maarifa kinywani mwake (Malaki 2:7), nakuhudumia Uzao halisi kwa haki, hiyo ndiyo Ibada.
Wewe unayesoma ujumbe huu ukiwa ofisini, na ofisi hiyo uliipata kwa haki na kila anayekuja unamhudumia kwa haki, hiyo ndiyo Ibada, nakadhalika.
Katika kuhitimisha, tuelewe kuwa sijasema Mitume, na Manabii wabomoe nyumba zao za Ibada; bali nimesema kuwa twende kwenye Nyumba za Ibada kwa ajili ya kumrudishia CHANZO HALISI sifa, heshima, shukrani na utukufu (Isaya 42:8) kwa kutuwezesha kuzalishaji na kupata utajiri udumuo; huku tukijua kuwa ibada hasa ni ile tunayoifanya wakati wa uzalishaji.
Karibuni wote.