Katibu Mkuu wa Nishati ataka michezo itumike kuboresha afya, ufanisi kazini

Na Zuena Msuya, Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja ameiasa Timu ya Wanamichezo wa Wizara ya Nishati inayoshiriki Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI), kutumia michezo hiyo kama sehemu ya kuboresha afya na ufanisi sehemu za kazi.
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja (wa tano kushoto) akikabidhi mpira kwa Mwenyekiti wa Michezo wa Wizara ya Nishati, Germanus Haule (wa nne kushoto), mara baada ya kutoa nasaha kwa wanamichezo hao, Oktoba 18,2021 jijini Dodoma, wa tano kulia ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu wa wizara hiyo, Ziana Mlawa. (Picha na Zuena Msuya-WN).

Mhandisi Masanja amesema hayo mkoani Dodoma wakati akitoa nasaha kwa wachezaji hao wanaokwenda kushiriki SHIMIWI mkoani Morogoro kuanzia Oktoba 20 hadi Novemba 2, 2021.

Aidha, amewataka wanamichezo hao kuheshimu michezo hiyo na kuzingatia dhana nzima ya kuanzishwa kwake.

Vilevile amewasihi wanamichezo hao kucheza kwa nidhamu pamoja na kuwa na mbinu za ziada ili kupata ushindi wa kishindo.

Sambasamba na hilo amewaeleza kuwa wanapokuwa kambini wanapaswa kuishi kwa nidhamu kwa mujibu wa Sheria za Utumishi wa Umma.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu wa Wizara ya Nishati, Ziana Mlawa (katikati) akizungumza na wanamichezo wa wizara hiyo (hawapo pichani) walipokuwa wakipatiwa nasaha kabla ya kwenda kushiriki Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI), mkoani Morogoro
Mwenyekiti wa Michezo wa Wizara ya Nishati, Germanus Haule (aliyesimama) akiwaeleza jambo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Wizara ya Nishati Ziana Mlawa (mwenye kilemba) kabla ya kupewa nasaha za kwenda kushiriki Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI),mkoani Morogoro Oktoba 18,2021.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa wizara hiyo, Ziana Mlawa amewaeleza wanamichezo hao kuwa wanapokuwa kambini ni sawa na wanapokuwa maeneo yao ya kazi hivyo wafuate na kuzingatia taratibu zote za kiutumishi.

Mlawa amesema kuwa, wanamichezo hao wakawe mfano bora kiutendaji kwa kushiriki mazoezi ya aina yote na yale yote wanayopaswa kufanya wanapokuwa katika michezo hiyo.

Vilevile amewasihi kuendeleza umoja, ushirikiano kwa wanamichezo wote watakaokuwa pamoja kama wanavyoshirikiana na watumishi wengine katika wizara ya Nishati.

Takribani wanamichezo 30 kutoka vitengo na idara za wizara hiyo watashiriki michezo ya Mpira wa Pete, Miguu, kuvuta kamba, kuendesha Baiskeli, mbio za Magunia na mingine.

Michezo ya SHIMIWI inatarajiwa kufunguliwa Oktoba 20, 2021 na kufikia kilele chake Novemba 2, 2021 mkoani Morogoro.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news