NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Hamisi Shabani (25) mkazi wa Mtaa wa Mizani,Kata ya Mandewa Halmashauri ya Manispaa ya Singida amehukumiwa maisha jela baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Singida kumtia hatiani kwa makosa ya kubaka pamoja na kulawiti.
Colesta Benedicta ambaye ni Mwanasheria wa Serikali alidai pia kwamba Mahakama hiyo imemuhukumu adhabu ya kifungo cha nje cha mwaka mmoja,Shabani Rajabu (17) mkazi wa Mtaa wa Mizani katika Manispaa ya Singida baada ya kumtia hatiani kwa makosa ya kubaka na kulawiti.
Ilidaiwa na Mwanasheria huyo wa serikali kwamba Mahakama hiyo imelazimika kumfunga kifungo cha nje Shabani Rajabu kutokana na kusimamiwa na Sheria ya Watoto kutokana na umri wake kutofikia miaka 18.
Benedicta alidai kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 27, 2020 majira ya saa za usiku,kwenye mtaa wa Mizani,Kata ya Mandewa,Manispaa ya Singida ambapo mshitakiwa huyo alikuwa akiishi nyumba moja na kupanga na mwanamke huyo waliyembaka na kumlawiti.
Mwansheria huyo alidai pia kwamba siku ya tukio mshitakiwa huyo na mwenzake waliokuwa wakiishi nyumba moja ya kupanga na mwanamke huyo (jina limehifadhiwa) alinunua pombe ya kienyeji na kisha kumkaribisha mwanamke na kuanza kunywa pamoja hadi alipolewa.
Benedicta alidai pia kuwa baada ya Hamisi Shabani kumaliza kufanya tendo hilo alimkaribisha na Shabani Rajabu ambaye naye alishiriki kufanya tendo hilo.
Kwa mujibu wa Mwanasheria huyo washitakiwa hao baada ya kusomewa mashitaka yao walikana na ndipo Mahakama hiyo ilipeleka mashahidi saba waliotoa ushahidi ambao haukuacha shaka yeyote ile kuwa washitakiwa hao ndio waliotenda kosa hilo na kuwaona wana makosa.
Akitoa hukumu ya kesi ya jinai namba 168/2020,Hakimu Mkazi Mwandamizi,Robert Oguda alisema ili liwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama ya washitakiwa hao,hivyo ilimuhukumu,Hamisi Shabani adhabu ya kutumikia kifungo cha maisha jela.
Aidha, Hakimu Oguda hata hivyo alisisitiza kwamba kutokana na umri wa Shabani Rajabu kutofikia miaka 18 na kwa kuwa mshitakiwa huyo anasimamiwa na sheria ya watoto,hivyo Mahakama hiyo ilimuhukumu kutumikia adhabu ya kifungo cha nje cha mwaka mmoja.