NA MWANDISHI DIRAMAKINI
WAKATI Timu ya soka ya KMC ikiikaribisha Timu ya Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara hapo kesho katika uwanja wa Majimaji mjini Songea,Serikali mkoani Ruvuma imewataka wapenzi na washabaki watakaofika kushuhudia mchezo huo kuchukua tahadhari dhidi ya Ugonjwa wa Covid-19.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amesema hayo, wakati akiongea na Waandishi wa Habari na viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu mkoani humo (Faru) ofisini kwake mjini Songea.
Jenerali Ibuge amesema, Serikali ya mkoa imefanya maandalizi yote kuhakikisha kuna kuwa na amani na utulivu kwa wapenzi na washabaki wa ndani na nje ya mkoa wa Ruvuma watakaokuja kushuhudia mchezo huo, hata hivyo ni vyema wakachukua tahadhari ili kuepuka kuambukizwa Covid -19.
Ametoa wito kwa wananchi ambao bado hawajapa chanjo,kwenda katika vituo vilivyotengwa kwa ajili ya kupata chanjo kabla ya kuingia uwanjani ili kujikinga na kuepuka uwezekano wa kuambukizwa kwa urahisi.
Ameuagiza uongozi wa Chama cha Soka mkoa na TFF kuhakikisha wanaweka vifaa vyote muhimu ikiwemo maji tiririka yenye sabuni ambapo kila mshabiki atakayeingia uwanjani lazima anawe mikono na kuvaa barakoa.
“Mchezo huu utachukua idadi kubwa ya watu,kwa hiyo ni lazima serikali tuhakikishe tunachukua hatua ya kudhibiti uwezekano wa watu kupata maambukizi ya virusi vya korona,Tff akikisheni mnaweka vifaa vyote muhimu na mazingira ambayo rafiki,”amesema Ibuge.
Aidha Mkuu wa mkoa,amewakaribisha wananchi hususani wapenzi wa mpira wa miguu wa Ruvuma na mikoa jirani ya Nyanda za juu kusini, kuja kwa wingi kushuhudia mchezo huo utakaoanza majira ya saa tisa jioni na kuwataka watoa huduma kuhakikisha wanaboresha huduma zao kwa wageni.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoa wa Ruvuma Kamwanga Tambwe, ameishukuru Klabu ya KMC kwa kuchagua uwanja wa Majimaji kuwa wa nyumbani na kuhaidi kwamba watatoa ushirikiano kwa timu hiyo na timu nyingine zitakazo amua kuja kucheza michezo yake Ruvuma.
Kwa upande wake,katibu wa Timu ya KMC Walter Harson amesema, wamejiandaa kushinda katika mchezo huo na kuwataka wapenzi wa mpira wa miguu mkoani Ruvuma kuiunga mkono Timu hiyo.
Amesema, katika mchezo dhidi ya Yanga wameweka viingilio rafiki Sh.7000 mzunguko na Sh.10,000 jukwaa kuu ili kutoa fursa kwa watu wengi kwenda kushuhudia mchezo huo.
Pia amesema, baada ya mechi na Yanga wataangalia uwezekano wa kutumia uwanja wa Majimaji kama uwanja wao wa nyumbani katika mchezo wake na Timu ya Simba ambao utafanyika Mwezi Desemba.
Tags
Michezo