Na Yusuph Mussa, Lushoto
KAIMU Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga Lucy Maliyao amesema zoezi la chanjo Awamu ya Kwanza limekwenda vizuri kwa watu 2,941 kujitokeza kuchanja chanjo ya UVIKO 19 na kuweza kuhitimisha zoezi hilo Oktoba 11, 2021.
Mkuu wa Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga Kalisti Lazaro (kushoto) akishuhudia mmoja wa wananchi wa Kata ya Gare akipata chanjo ya ugonjwa wa UVIKO 19 kutoka kwa Ofisa Muuguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Veronica Shehiza (kulia). (Picha na Yusuph Mussa).
Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga Lucy Maliyao akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake Oktoba 12, 2021. (Picha na Yusuph Mussa).
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Oktoba 12, 2021 ofisini kwake, Maliyao alisema walipokea chanjo 3,450, lakini kutokana na sababu za kitabibu waliweza kuchanja wananchi 2,941, huku chanjo 509 zikiharibika.
Alisema wameweza kukamilisha zoezi hilo kwa ufanisi baada ya makundi mbalimbali kwenye jamii kupata elimu ya ugonjwa wa UVIKO 19 na faida ya chanjo yenyewe, ambapo elimu hiyo ilianza kutolewa kwanza kwa wahudumu wa afya, baadae watumishi wa idara mbalimbali ngazi ya halmashauri, viongozi wa Serikali ngazi ya kata, vijiji, viongozi wa dini na wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga Kalisti Lazaro (wa pili kushoto) akishuhudia mmoja wa wananchi wa Kata ya Migambo akipata chanjo ya ugonjwa wa UVIKO 19 kutoka kwa Ofisa Muuguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Veronica Shehiza (kulia). Kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Lushoto Shaaban Shekilindi 'Bosnia' (Picha na Yusuph Mussa).
Ofisa Muuguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Theodora Tesha akitoa chanjo ya ugonjwa wa UVIKO 19 kwa mmoja wa wanafunzi wa mafunzo ya mgambo Kata ya Kwekanga. (Picha na Yusuph Mussa).
Dereva Mstaafu wa Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Rupia Mlyuka akipata chanjo ya UVIKO 19 kutoka kwa Ofisa Muuguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Veronica Shehiza. Chanjo hiyo ilifanyika Kata ya Ngulwi. (Picha na Yusuph Mussa).
"Tulipata chanjo 3,450 , waliochanjwa ni wananchi 2,941 na chanjo zimeisha. Kulikuwa na vituo vya chanjo 41, ambapo hospitali ilikuwa moja, vituo vya afya vitano na zahanati 35. Mkuu wa Wilaya ya Lushoto (Kalisti Lazaro) alikuwa na mchango mkubwa kwenye kuhamasisha zoezi la chanjo, kwani kwenye mikutano yake aliyoifanya kwa siku nane kwenye halmashauri yetu, wananchi waliojitokeza kuchanja ni 498 wastani wa wananchi 62 hadi 63 kwa siku.
"Lakini pia zoezi hilo limefanikiwa kwa kutoa elimu kwa wasimamizi wa afya ngazi ya halmashauri na watumishi wa idara zote ngazi ya halmashauri ambao pia walipewa chanjo. Lakini pia tulitoa elimu kwa wahudumu wa afya ikiwemo vituo vya afya, zahanati na hospitali. Pia kulikuwa na madiwani, watendaji wa kata na watendaji wa vijiji yalipo makao makuu ya kata, watoa Huduma ya Afya kwenye Jamii (CHW), shule za sekondari, magereza, viongozi wa dini, pia misikitini na kanisani" alisema Maliyao.
Maliyao ambaye ni Muuguzi Mkuu (DNO) wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, alisema moja ya changamoto ilikuwa ni uelewa mdogo wa wananchi kuhusu ugonjwa wa UVIKO 19 na umuhimu wa chanjo yenyewe, kwani elimu bado inahitajika zaidi hasa watakapopokea chanjo ya Awamu ya Pili hivi karibuni.