Maagizo ya Waziri Mchengerwa kwa viongozi na watumishi wa umma

Na James K. Mwanamyoto,Mwanza

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Viongozi na Watumishi wa Umma kuwajibika kikamilifu katika kutatua kero na changamoto zinazowakabili wananchi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na Watumishi wa Umma wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kituo cha Kumbukumbu Kanda ya Ziwa jijini Mwanza.

Mhe. Mchengerwa ametoa maelekezo hayo wakati akizindua Kituo cha Kumbukumbu Kanda ya Ziwa kilichopo jijini Mwanza.

Mhe. Mchengerwa amesema, Watanzania wapo zaidi ya milioni 60 na kila mmoja anatamani kufanya kazi Serikalini lakini hawajapata nafasi hiyo, hivyo ni vema waliobahatika kupata nafasi hiyo kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

“Nikiwa Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ninawaagiza kila mmoja wetu awajibike na kuguswa katika kutatua kero zinazowakabili wananchi,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza na kuongeza kuwa, Viongozi na Watumishi wa Umma hawawezi kuwa na uhalali wa wa nafasi zao iwapo hawajishughulishi na kero za wananchi kwani wananchi hao ndio wenye serikali.

Mhe. Mchengerwa amesema, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan inathamini sana wananchi wake, hivyo Viongozi na Watumishi wa Umma kwa nafasi zao waiunge mkono kwa vitendo ili kujenga imani ya wananchi kwa serikali yao.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Amina Makilagi akielezea namna Serikali ya Awamu ya Sita inavyowajali wananchi wake katika kuwaondolea umaskini kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kituo cha Kumbukumbu Kanda ya Ziwa jijini Mwanza.
Sehemu ya Watumishi wa Umma kutoka Taasisi za Serikali wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao kwenye hafla ya uzinduzi wa Kituo cha Kumbukumbu Kanda ya Ziwa jijini Mwanza.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watendaji wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Utumishi wa Umma na Utawala Bora baada ya Mhe. Mchengerwa kuzindua Kituo cha Kumbukumbu Kanda ya Ziwa jijini Mwanza.

Akizungumzia mchango wa Serikali katika kuwajali wananchi, Kaimu Mkuu wa Mkoa ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mhe. Amina Makilagi amesema Serikali kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini imewanufaisha wananchi 58,000 ambao wamepata ruzuku ya zaidi ya shilingi bilioni 61 ambazo zimepokelewa toka Awamu ya Kwanza ya TASAF.

Sanjali na hilo, Mhe. Makilagi amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa TASAF Awamu ya Tatu Kipindi cha Pili ambapo hivi karibuni fedha zitaanza kupelekewa kwa walengwa.

Serikali imetenga kiasi cha shilingi trilioni 2 na bilioni 300 ambazo zitawezesha kuzifikia kaya zote maskini zenye sifa za kunufaika na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news