NA DOREEN ALOYCE
BARAZA la Madiwani wa Jiji la Dodoma limeahidi kusimamia vyema fedha shilingi 2,974,672,970.48 zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa ajili utekelezaji wa miradi ya mpango wa maendeleo ya ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye Baraza lao la Madiwani leo wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa fedha hizo ambapo kwa Jiji la Dodoma wamepewa kiasi kikubwa.
Wamesema kuwa, kwa ushirikiano wa Mkurugenzi wa Jiji hilo, Joseph Mafuru watahakikisha wanasimamia fedha hizo katika utekelezaji wa miradi iliyokusudiwa.
"Kiukweli tunamshukuru sana Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kutujali Watanzania hasa hizi pesa zilizotolewa nchi nzima ambazo zimejizatiti kutekeleza miradi hasa madarasa,barabara, hospitali,maji na miundombinu mbalimbali ikiwemo ujenzi wa uwanja wa ndege,"wamesema.
Wamesema kuwa, Rais ameonyesha kutimiza ile miradi aliyoacha Hayati John Magufuli na kwamba miradi hiyo italeta matokeo chanya kwa wananchi na kwamba fedha hizo zinapaswa kuwa za uwazi ili miradi iweze kutekeleza kwa wakati.
Edward Magawa ni Diwani wa Kata ya Ihumwa amesema kwamba, kwa miaka mingi suala la madarasa limekuwa changamoto katika kata mbalimbali za Jiji la Dodoma jambo ambalo limepelekea wanafunzi kusoma katika mazingira magumu na kwamba watahakikisha wanasimamia kwa uaminifu miradi hiyo.
Diwani wa Kata ya Kizota, Jamary Yaredi amesema kuwa, katika kata yake amepewa zaidi ya milioni 140 kwa ajili ya madarasa katika shule ya msingi na sekondari ambazo zitaondoa changamoto ya upungufu wa madarasa hayo ambapo alidai kwa sasa tayari anawasiliana na watu wa mamlaka wa barabara za vijijini TARURA kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara na mitaro.
Awali akiongea katika baraza hilo la Madiwani, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alisema kuwa, tayari baraza hilo limelenga kuweka mikakati na madiwani hao juu ya kusimamia vyema fedha ambazo tayari zimetengwa kwenye kila kata kutekeleza miradi hiyo.
"Tunamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupendelea Jiji la Dodoma kutoa fedha nyingi, Halmashauri inaahidi kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo na matumizi sahihi ya fedha na tunaamini ndani ya mwezi mmoja kama tulivyoelekezwa Tutakuwa tumekamlisha na watakaoenda kinyume nanmatumizi ya fedha hizo watachukuliwa hatua kali za kisheria,"amesema Mafuru.
Akifafanua fedha hizo amesema, zimejigawa kwenye ujenzi wa madarasa ya sekondari idadi 143 ambayo itakagharimu 2,860,000,000.00, ujenzi wa madarasa ya vituo shikizi vinne kwa shilingi 80,000,000.00, pamoja na kampeni ya Chanjo dhidi ya UVIKO-19 kiasi cha shilingi 34,672,970.48.
Katika hatua nyingine, Mafuru kwenye baraza hilo alisema, kufuatia changamoto ya machinga katika Jiji la Dodoma kwamba tayari kumetengwa eneo kubwa kwa ajili yao ili waweze kufanya shughuli zao kwa ufanisi.
"Tumetenga eneo katika mtaa wa Bay road ambapo kulikuwa kuna paki magari ya maroli, lakini kwa sasa tumetenga stendi ya magari hayo jambo ambalo tumejadili na kuona eneo hilo liwe la wamachinga ili waweze kufanya shughuli zao kwa ufanisi.
"Na kwa sasa tayari tumepeleka wataalamu kukagua eneo na hivi karibuni ujenzi wa eneo hilo unaanza mara moja na kikubwa zaidi tutaweka miundombinu yote ya kufanya biashara zao bila bugudha ikiwemo sehemu ya wamama kunyonyeshea watoto wao,"amesema Mkurugenzi Mafuru.
Awali akizungumza katika baraza hilo, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Jabiri Shekimweri alitumia nafasi hiyo kuwasihi kutumia fedha hizo kwa ufanisi na kutekeleza muongozo na mchanganuo uliotolewa na Ofsi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ukazingatiwe ambapo kila diwani anapaswa awe na nakala yake.
"Sisi kazi yetu tutahakikisha tunafanya ziara za ukaguzi wa mara kwa mara, kujua kazi inavyoendelea ili lengo la Rais liweze kutimia kwa haraka, hivyo madiwani niwasihi mtekeleze na kusimamia miradi hiyo kwa umakini mkubwa,"amesema Shekimweri.
Aidha, amewataka madiwani kuacha kujadili vitu vyepesi ambavyo vinaweza kuongeleka na wataalamu wao ofisini na badala yake wajikite kurudi kwenye hoja za msingi za kusukuma maendeleo ya Jiji mbele na wananchi zikiwemo namna ya kutatua migogoro ya ardhi na sio hoja za mtu binafsi.