Na Mwandishi Wetu, Iringa
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Iringa Mjini mkoani Iringa, Joseph Mgongolwa amewataka wanachama wa chama hicho tawala kuacha makundi na kuwa wamoja ili kuwezesha ustawi bora wa chama na ushindi katika chaguzi mbalimbali zijazo.
Pia amewataka wana CCM na Watanzania kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwani ameonesha uwezo mkubwa wa kiuongozi na anatosha kuendelea hata baada ya mwaka 2025.
"Makundi ni ugonjwa hatari sana ndani ya chama ni sawa na ukoma maana wanapoibuka watu wachache na kuanza kujipanga kwa ajili ya fulani wanatengeneza matabaka ambayo yanaweza kudhoofisha uimara wa chama, hivyo kukisababishia maumivu siku za usoni.
"Sisi wana CCM tunapaswa kuwa wamoja, kuwaunga mkono waliopewa dhamana na kushirikiana nao bega kwa bega ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi, hatua ambayo itakiwezesha chama siku zijazo kikisimamisha mgombea yoyote asipate kipingamizi hususani katika uchaguzi mkuu ujao. Tuendelee kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwani anatosha na ana uwezo mkubwa wa kiuongozi;
Mgongolwa aliyasema hayo jana mjini hapa wakati akizungumzia namna ambavyo amejipanga kuendelea kuhamasisha umoja na mshikamano kwa wana CCM ili waendelee kushiriki kukijenga chama chao ikiwemo kuunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ili iweze kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa ufanisi.
Alisema kuwa, umoja na mshikamano ni nguzo muhimu katika kuiwezesha Serikali iliyopo madarakani iweze kutekeleza ipasavyo ilani hiyo ya 2020 hadi 2025 ambayo imeangazia mambo mbalimbali kwa ustawi bora wa taifa letu na jamii kwa ujumla.
Mjumbe huyo alisema kuwa, iwapo wana CCM watayazima makundi yao na kuwa kitu kimoja watarajie kupiga hatua kubwa katika chaguzi zijazo sambamba na utekelezaji wa ilani kwa ufanisi.
"Kwa sababu makundi yanapojengeka iwe kwa waliopewa dhamana ambao wakati mwingine fikra zao zinawaza chaguzi zijazo au wale ambao hawakufanikiwa ndani ya chama yanachangia kwa kiwango kikubwa kukwamisha juhudi za Serikali kupiga hatua, tuwe kitu kimoja na tuendelee kuiunga mkono Serikali yetu sikivu iweze kuwaletea wananchi maendeleo,"alisema.
Wakati huo huo, Mgongolwa amempongeza Rais Samia kwa kazi nzui anazoendelea kuzifanya kwa ajili ya kulijenga Taifa letu katika nyanja za kiuchumi, kijamii ikiwemo ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo inaendelea katika kila kona ya nchi.
Kazi iendeleeee
ReplyDelete