Serikali yadhamiria kuja na suluhu ya udumavu katika mikoa inayoongoza kwa uzalishaji mazao

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Serikali imeahidi kuwekeza kwenye tafiti za kina kutafuta sababu za kuongezeka kwa udumavu kwenye mikoa inayoongoza kwa uzalishaji mkubwa wa vyakula vinavyotakiwa kwenye ukuaji wa watoto.
Pia taasisi za utafiti wa mazao nchini zimetakiwa kuongeza jitihada katika kuhamasisha kilimo cha mbegu bora na kwa njia za asili ili kuongeza ufanisi na lishe bora kwa rika zote.

Steven Kagaigai ambaye ni mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro ameema hayo wakati akizindua Siku ya Chakula Duniani inayofanyika kitaifa mkoani Kilimanjaro katika viwanja vya Shule ya msingi Mandela mjini Moshi.

Amesema, Serikali kupitia taasisi zake za utafiti nchini na kwa kushirikiana na wadau wa kitaifa na kimataifa itaongeza nguvu katika tafiti mbalimbali, lakini pia katika utafiti huu wa kutafuta sababu za ongezeko la udumavu kwenye mikoa yenye uzalishaji mzuri wa vyakula.

"Tuna hali nzuri sana ya uzalishaji wa chakula hapana nchini kiasi cha kwamba tumeruhusu uuzaji wa mazao nje ya nchi, lakini ni muhimu kuwakumbusha tunapaswa kuhifadhi vyakula kwa ajili ya matumizi yetu kama miongozo inavyosema,"amesema.

Mkuu wa mkoa amesema, mahitaji ya chakula nchini kwa mwaka 2021/22 ni tani 14,796,751 ikiwa ni ziada ya tani 3,628496, hivyo hakuna athari iwapo watanzania watauza mazao yao kwa masoko ya ndani na nje ya nchi.

Awali Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt.Godwin Mollel alitaja mikoa inayoongoza kwa udumavu nchini kuwa ni Songwe, Mbeya, Iringa na Ruvuma na kwamba kuna kila sababu kutafuta chanzo cha udumavu licha ya kuongoza kwa uzalishaji chakula.

Naibu Waziri huyo alizitaka mamlaka nyingine ikiwemo ya TFDA, kuwasaidia wakulima ili waweze kuongeza thamani ya mazao yao ili wapate vibali mapema hivyo kuwasaidia watanzania kupata lishe bora.

Aidha, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mwaka jana katika maadhimisho kama hayo, ilibainishwa kuwa Njombe ilikuwa na udumavu wa asilimia 53.6 wakati uzalishaji mazao ni tani 446,49, ikifuatiwa na mkoa wa Rukwa ambao ulikuwa na udumavu wa asilimia 47.9 huku uzalishaji ukiwa ni tani 943,002 na kiwango cha Utoshelevu-SSR asilimia 230.

Kwa upande wa Iringa ulikuwa na udumavu wa asilimia 47.1, huku uzalishaji ni tani 470,750 na kiwango cha utoshelevu-SSR asilimia 161 ikifuatiwa na Songwe ilikuwa na udumavu asilimia 43.3 huku uzalishaji mazao ni tani 805,545 na kiwango cha utoshelevu cha asilimia 210.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news