NA MWANDISHI MAALUM, PSC
Mkutano wa Kwanza wa Tume ya Utumishi wa Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 unatarajiwa kuanza siku ya Jumatatu tarehe 25 Oktoba 2021 na kumalizika tarehe 12 Novemba 2021 jijini Dodoma.
Mkutano huu utaongozwa na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma Mheshimiwa Jaji Rufaa (Mst.) Dkt. Steven J. Bwana.
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma Bw. Mathew M. Kirama, kupitia taarifa iliyotolewa leo na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini cha Tume hiyo, amesema kuwa katika Mkutano huu Tume itapokea, itajadili na kutolea uamuzi Rufaa na Malalamiko mbalimbali yaliyowasilishwa Tume na Watumishi wa Umma ambao hawakuridhika na uamuzi uliotolewa na Waajiri, Mamlaka za Ajira na Mamlaka zao za Nidhamu.
Bw. Kirama amesema kuwa shughuli nyingine zilizopangwa kufanyika wakati wa Mkutano huu ni pamoja na kupokea na kujadili taarifa mbalimbali za utekelezaji wa Majukumu ya Tume na Mpango Mkakati wa Tume ya Utumishi wa Umma kwa kipindi cha mwaka 2021/2022 hadi 2025/2026.
Tume ya Utumishi wa Umma inatekeleza majukumu haya kwa mujibu wa Kifungu cha 10(1) cha sharia ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298.
Tags
Habari