NA FRESHA KINASA
Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Mwalimu Makuru Lameck Joseph amesema kuwa, juhudi zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan za kukuza uchumi wa Watanzania zinapaswa kuthaminiwa na kuungwa mkono na kila mtu, kwani zina lengo la kuistawisha nchi pamoja na kuzifanya rasilimali zilizopo zihakisi maisha ya Watanzania.
Amesema Rais ana dhamira ya dhati ya kufufua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na uchumi jumuishi kutokana na miradi mbalimbali ya kimkakati ambayo amedhamiria kuitekeleza na hivyo fedha nyingi zitawarudia wananchi na kuwanufaisha moja kwa moja ama kupitia huduma za kijamii.
Ameyasema hayo leo Oktoba 26, 2021 wakati akizungumza na DIRAMAKINI BLOG Mjini Musoma katika mahojiano maalum.
Mwalimu Makuru amesema, Rais Samia ana shauku kubwa ya kuinua maisha ya Watanzania na ndio maana amekuwa mstari wa mbele kutafuta fedha ambazo zinawezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo Shilingi trilioni 1.3 za Mpango wa Maendeleo na mapambano dhidi ya UVIKO-19 zilizopatikana kutokana na juhudi zake na hivyo ameomba juhudi hizo ziungwe mkono na kuthaminiwa, kwani zina tija kwa taifa.
"Sote tunaendelea kuona juhudi thabiti zinazofanywa na Rais Samia Hassan katika kuhakikisha kwamba maendeleo yanapaa katika nchi yetu. Rais ameendelea kutafuta fedha, hii yote ni kwa ajili ya Watanzania.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Oktoba 10, 2021 akizindua Mpango wa Serikali wa Kuinua Uchumi na kukabiliana na janga la Korona, UVIKO-19 wenye thamani ya shilingi Trilioni 3.62 katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma. (Picha na Maktaba).
"Pia tumeona fedha zinazokusanywa kutokana na tozo zinawarudia Watanzania ikiwemo kujenga vituo vya afya na madarasa, juhudi hizi zithaminiwe na Rais aungwe mkono kwa mikakati yake thabiti,"amesema Mwalimi Makuru.
"Hivi sasa madarasa yanakwenda kujengwa katika shule mbalimbali nchini pamoja na vituo vya afya kutokana na fedha hizo. Jambo hili ni la kipekee sana na la kihistoria katika Taifa letu. Lazima Rais Samia Hassan tumpongeze kwa dhati kwa ushupavu wake aliouonesha, kwani umemfanya aguse kwa kiwango kikubwa sana maisha ya wananchi sasa uhaba wa madarasa utakwisha na wanafunzi watasoma kwa ufanisi mkubwa," amesema Mwalimu Makuru.
Kutokana na hatua hiyo, Mwalimu Makuru amewaomba viongozi wa Serikali kusimamia vyema fedha hizo kusudi zifanye kazi iliyokusudiwa na kwamba miradi itakayotekelzwa iendane na thamani ya fedha hizo, kwani usimaizi mzuri utawezesha utekelezwaji wa miradi kwa ufanisi na kukidhi matarajio ya Rais na Serikali kwa ujumla.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akipokea chanjo dhidi ya Uviko-19 hivi karibuni. (Picha na Maktaba).
Mbali na hayo, Mwalimu Makuru amesema, hatua ya Rais Samia kuwaongoza Watanzania kupata Chanjo ya UVIKO-19 ni ishara ya kwamba nia yake ni kuona Watanzania wanakuwa na siha njema na kwamba wanajikinga na ugonjwa huo. Ambapo amesisitiza Watanzania kuendelea kujitokeza kuchanja, kwani kwa kufanya hivyo ni kushiriki kikamilifu katika mapambano ya UVIKO-19 kama ambavyo Serikali imekusudia.
"Nia ya Serikali ni kuona Watanzania wanakuwa na afya njema, ndio maana chanjo ya Corona inatolewa ili wananchi wachanje na wajikinge na Corona. Mtu asipokuwa na afya njema hawezi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali. Juhudi hizi za Rais kutaka Watanzania wawe salama lazima ziungwe mkono na kupongezwa na makundi yote katika Taifa letu,"amesema Mwalimu Makuru.
Pia, Mwalimu Makuru amesema, kitendo cha Rais Samia alichokifanya cha kuandaa kipindi maalumu kwa ajili ya kutangaza fursa zitokanazo na sekta ya utalii nchini cha Royal Tour ni ishara kubwa ya uzalendo na uwajibikaji wake kwa maslahi ya nchi na kutaka kuona rasilimali hizo zinaleta mapinduzi chanya ya kiuchumi kwa wananchi wake, jambo ambalo lina faida kwa nchi, kwani taifa litapata watalii na wawekezaji ambao watakuwa chachu ya maendeleo ya nchi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa amejumuika na wananchi jijini Zanzibar katika siku za karibuni wakati akirekodi kipindi maarufu cha Royal Tour chenye lengo la kuitangaza Tanzania kimataifa. (Picha na Maktaba).
Katika hatua nyingine, Mwalimu Makuru amewaomba Watanzania wote kuendelea kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan kusudi aweze kufanikisha mipango yake kwa ufanisi ya kuwaletea maendeleo Watanzania.