NA MUNIR SHEMWETA, WANMM
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula amefanya ziara ya kushtukiza ofisi ya ardhi ya halmashauri ya jiji la Dodoma na kuagiza maombi 521 ya umilikishaji ardhi katika ofisi hiyo kukamilishwa ndani ya siku tatu.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akipata maelezo kutoka kwa Afisa Ardhi Mteule Halmashauri ya Jiji la Dodoma Pirmin Mzenga alipofanya ziara ya kushtukiza ofisi za ardhi za jiji la Dodoma tarehe 25 Oktoiba 2021. Kushoto ni Kamishna wa Ardhi nchini Nathaniel Nhonge.
Akiwa ameambatana na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Mary Makondo na Menejimenti ya Wizara katika ziara hiyo tarehe 25 Oktoba 2021 jiji Dodoma, Dkt Mabula alisema, pamoja na kuwepo changamoto lakini anachohitaji maombi 521 yawe yamekamilika katika kipindi cha siku tatu.
‘’Kuanzia sasa tunahitaji zile ‘application’ zote ambazo hati zake watu wameomba zitoke ndani ya siku tatu kama ni kutoka saa nane za usiku tunahitaji hiyo kazi ikamilike ndani ya siku tatu,’’ alisema Dkt Mabula.
Aidha,aliwataka watendaji wa sekta ya ardhi katika jiji la Dodoma kuandaa hati zisizopungua mia moja kwa siku moja sambamba na kuwataka kumhakikishia kwa maandishi ahadi walizompa katika kutekeleza maagizo yake.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi kwenye halmashauri ya jiji la Dodoma wakati wa ziara ya kushtukiza ofisi za ardhi za jiji la Dodoma tarehe 25 Oktoba 2021. Wa pili Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Mary Makondo.
Uamuzi wa Naibu Waziri wa Ardhi kufanya ziara ya kushtukiza ofisi ya ardhi katika jiji la Dodoma unafuatia kujitokeza baadhi ya malalamiko ucheleweshaji umilikishaji ardhi kwa wananchi wa mkoa wa Dodoma jambo lililofanya wizara kuanza mkakati maalum wa ukwamuaji na uharakishaji utoaji hati kwenye jiji hilo.
Awali Naibu Waziri Dkt Mabula na timu yake walitembelea vitengo vya ardhi katika halmashauri ya Jiji la Dodoma ili kubaini baadhi ya changamoto katika sekta hiyo.
Dkt.Mabula alisema, jiji la Dodoma ndiyo sura ya nchi hivyo Maafisa wake wa ardhi wanatakiwa kuwapanga wananchi wanaokwenda kupata huduma kulingana na maeneo wanayotoka sambamba na maafisa hao kuvaa vitambulisho ili kutambulika kwa wananchi.
‘’Hatuihitaji kusikia kelele za watu hapa, ninyi mnachafua image ya Wizara na sekta kwa sababu tu ya kutojipanga kwenye utendaji wenu wa kazi, mko wengi mnaweza kujipanga vizuri pamoja na kuwepo upungufu wa watumishi kwa baadhi ya maeneo,’’ alisema Dkt Mabula.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akipata maelezo kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Urasimishaji Makazi Paulo Kitosi alipofanya ziara ofisi ya Ardhi mkoa wa Dodoma tarehe 25 Oktoba 2021. Kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Mary Makondo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo alieleza kuwa, wizara yake imejipanga kuhakikisha inaongeza kasi ya umilikishaji ardhi katika mkoa wa Dodoma na Maeneo mengine nchini.
Katika jitihada za ukwamuaji na kuongeza kasi ya utoaji hati katika jiji la Dodoma, Wizara yake imeamua kuongeza nguvu ya watumishi kutoka Makao Makuu ili kuharakisha kasi ya utoaji hati kwa wamiliki wa ardhi.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Ardhi Zakariyya Kerra (Aliyevaa miwani) pamoja na viongozi wengine wa Wizara baada ya kuhitimisha ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi kwenye mkoa wa Dodoma
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (Wa nne kushoto) na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Mary Makondo (wa tatu kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na Warasimu Ramani wa Wizara wakati wa ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Dodoma tarehe 25 Oktoba 2021.(PICHA ZOTE NA MUNIR SHEMWETA)
Kaimu Mkuu wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji Halmashauri ya jiji la Dodoma Amelyo Chaula aliweka wazi kuwa, mwamko mkubwa umilikishaji ardhi kutoka kwa wananchi umesababisha ofisi yake kuelemewa na kazi. Hata hivyo, alisema ofisi hiyo imekuwa ikifanya juhudi kubwa kuhakikisha wananchi wanapatiwa huduma kwa wakati pamoja na kuwepo changamoto kadhaa kwa baadhi ya maeneo hasa yale yaliyorithiwa kutoka iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA na kusisitiza kuwa maeneo mapya hayana changamoto ya Umilikishaji.