Na Happiness Shayo-WMU
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja amekagua ujenzi wa Hoteli ya Kitalii ya nyota tatu katika eneo la Lubambangwe Burigi wilayani Chato kwa lengo la kuangalia maendeleo ya ujenzi wa hoteli hiyo inayotarajiwa kutumika kwa ajili ya watalii watakaotembea maeneo ya vivutio vya Utalii Wilayani humo.
Amefanya ziara hiyo ya kushtukiza kutokana na kusuasua kwa ujenzi wa hoteli hiyo.
Mhe. Masanja amemuelekeza Mwakilishi wa Mradi huo kutoka TANAPA, Jeremiah Machibya kumsimamishia mkataba mkandarasi huyo kama ameshindwa kumaliza kazi kwa muda unaotakiwa.
"Kama mkandarasi kazi imemshinda tengueni mkataba muweke anayeweza kuimaliza kazi hii kwa wakati," Mhe. Masanja amesisitiza.
Mradi huo wenye gharama ya shilingi Bilioni 11 unaosimamiwa na TANAPA ulianza mwezi Aprili 2020 na ulitarajiwa kukamilika mwezi Aprili, 2021 lakini mkandarasi ameongezewa muda hadi mwezi Machi, 2022 na gharama za ujenzi zilizotumika mpaka sasa ni Bilioni 4.1.