NA ROTARY HAULE
Mkoa wa Pwani umepokea dozi nyingine aina ya Sinopharm 25,000 kwa ajili ya kuendelea na zoezi la chanjo ya awamu ya pili dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Gunini Kamba ameyasema hayo katika mkutano maalum wa kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo ya mkoa ikiwemo namna ya kukabiliana na ugonjwa huo uliofanyika Mjini Kibaha.
Kamba amesema kuwa, awamu ya kwanza walipokea chanjo 30,000 na zilimalizika kutokana na hamasa kubwa iliyofanyika na wananchi kujitokeza kuchanja kwa wingi.
Amesema kuwa,baada ya kumalizika kwa chanjo hizo walilazimika kuomba chanjo nyingine na hivyo kupata chanjo 25,000 za Sinopharm ambazo tayari zimeanza kutolewa Oktoba 25,2021.
Gunini amesema kuwa, chanjo ya Sinopharm haina tofauti na chanjo ya JJ isipokuwa chanjo ya Sinopharm inachomwa mara mbili ambapo inachukua muda wa siku 21 -28 kuchanja chanjo nyingine.
Ameongeza kuwa, tayari chanjo ya Sinopharm imetolewa katika halmashauri zote za Mkoa wa Pwani kwa kiwango tofauti na matarajio ni kuwa vitatumika vituo vyote 287 vilivyoanza kutumia awali.
"Kwa mujibu wa Serikali chanjo ya Sinopharm ilitakiwa kuanza kutolewa Oktoba 25 baada ya kufanyika kwa tathmini ya chanjo ya JJ na utaratibu wa utoaji wa chanjo ya Sinopharm unatakiwa uzingatie njia zilizotumika katika utekelezaji wa mpango wa Jamii Shirikishi na Harakishi.
Aidha,Kamba ameongeza kuwa, chanjo ya Sinopharm ni salama na inauwezo wa kusisimua mwili ukatengeneza kinga dhidi ya UVIKO-19 kwa asilimia 95 iwapo mlengwa atakamilisha dozi mbili huku akiongeza kuwa mtu yeyote kuanzia miaka 18 anaruhusiwa kuchanja.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inafanya kazi kubwa kwa ajili ya kuwakomboa wananchi wake.
Kunenge amesema ili kufika malengo ni lazima watendaji mbalimbali wahakikishe wanaunga mkono juhudi za Rais ili kuweza kufika mahali ambapo nchini inatakiwa kufika hususani katika kuiletea nchi maendeleo.
Kunenge amewataka Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na viongozi wengine wa ngazi mbalimbali kuhakikisha wanakwenda kuongeza hamasa na kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kujitokeza katika kupata chanjo hiyo.