Rais Samia amedhamiria kuboresha miundombinu-Waziri Mkuu

NA MWANDISHI MAALUM

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuboresha miundombinu ili Watanzania waendeshe shughuli zao kama za usafirishaji wa abiria na mizigo kwa urahisi na kukuza uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia wananchi katika kijiji cha Nandagala wilayani Ruangwa wakati alipokagua ujenzi wa barabara ya Nanganga-Ruangwa yenye urefu wa km 53.2.

“…endeleeni kutumia fursa za maendeleo zilizoletwa kupitia fedha za kodi katika kujipatia maendeleo na kukuza uchumi wenu kwani mna Serikali imara, Rais imara na wasaidizi wake wanafanya kazi usiku na mchana kwa ajili yenu.”

Ameyasema hayo Oktoba 25, 2021 baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Nanganga-Ruangwa (km 53.2) akiwa kwenye ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali mkoani Lindi.

Baada ya kukagua ujenzi wa barabara hiyo unaosimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Waziri Mkuu aliuagiza uongozi wa wakala huo usimamie vizuri mradi huo na uhakikishe inajengwa kwa viwango.
“TANROADS simamieni vizuri ujenzi wa mradi huu na mhakikishe barabara inajengwa kwa viwango na inakamilika kwa wakati. Mliopata ajira katika mradi huu fanyeni kazi kwa weledi hatutarajii kusikia mtu ameiba nondo wala saruji.”

Barabara hiyo inajengwa na kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Corporation ya China kwa gharama za shilingi bilioni 59.28 na imepangwa kukamilika Novemba 2022.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi, Rogatus Hussein Mativila alisema hadi kufikia mwezi Septemba mwaka huu ujenzi wa barabara hiyo ulikuwa umefikia asilimia 32.

Mhandisi Mativila alitaja kazi zilizofanyika katika mradi huo kuwa ni pamoja na kusafisha eneo la ujenzi, ujenzi wa kitako cha barabara, uinuaji wa tuta kwenye maeneo ya mabonde, ukataji wa maeneo yenye miinuko mikubwa na ujenzi wa makalavati.
Kipande cha barabara ya Nanganga – Ruangwa yenye urefu wa km 53.2 ambayo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikagua ujenzi wake katika eneo la Nandagala wilayani Ruangwa, Oktoba 25, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Kadhalika, Mtendaji Mkuu huyo alitaja barabara za mkoa wa Lindi ambazo Serikali imepanga kuzijenga kwa kiwango cha lami kuwa ni barabara ya Liwale-Nachingwea (km 130) ambayo ipo kwenye hatua ya kufanyiwa upembuzi yakinifu.

“Barabara ya Kiranjeranje-Namichiga-Ruangwa yenye urefu wa km 102 na barabara ya Masaninga-Nangukuru-Kilwa Masoko yenye urefu wa km 55 tayari zimeshafanyiwa tayari imeshanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina”

Akizungumzia kuhusu barabara ya Nangurukuru-Liwale Mhandisi Mativila alisema mkataba wa kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina tayari umeshasainiwa na kazi hiyo inatarajiwa kuanza ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news