Rais Samia atoa Bilioni 28.6/- ujenzi wa miradi ya maendeleo Geita

NA MWANDISHI MAALU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi bilioni 28.6 kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Geita.

Mheshimiwa Majaliwa amesema Rais Mheshimiwa Samia anataka kuona kila Mtanzania anapata huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo za afya, elimu, maji, nishati ya umeme na miundombinu katika makazi yao.

Ameyasema hayo Oktoba 12, 2021 wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Muganza katika wilaya ya Chato mkoani Geita. Alisema kati ya fedha hizo shilingi bilioni 16 zimepelekwa wilayani Chato. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia wananchi wa Kata ya Muganza, wilayani Chato, Mkoa wa Geita, Oktoba 12, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Mheshimiwa Majaliwa alitumia fursa hiyo kuwataka viongozi wa mkoa wa Geita kuhakikisha fedha hizo ambazo zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji, elimu, barabara na afya zinatumika kama ilivyokusudiwa.

Akizungumzia kuhusu changamoto ya upungufu wa watumishi wa sekta ya afya, Mheshimiwa Majaliwa alisema Serikali inaendelea kuajiri ili kuhakikisha lengo lake la kufikisha huduma bora za afya kwa wananchi linafikiwa.

Kadhalika, Waziri Mkuu aliuagiza uongozi RUWASA wilaya ya Chato uhakikishe kiasi cha shilingi bilioni 5.2 kilichotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa maji zinatumika vizuri na wananchi wapate huduma hiyo.

Mheshimiwa Majaliwa alitumia aliwaagiza viongozi hao wahakikishe wanaanza kufanya utafiti ili waweze kutumia maji ya Ziwa Victoria kwa kuyasambaza kwa wananchi. Alisema haiwezekani watu wanakaa karibu na ziwa na hawana maji ya kutosha.

Awali, Mbunge wa Chato, Dkt.Medrad Kalemani alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika wilaya hiyo kama ujenzi wa barabara, miradi ya ujenzi wa miundombinu ya elimu, vituo vya afya pamoja na miradi ya maji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news