ANAANDIKA RC DAVID KAFULILA...
Kwanza, kwa miongo kadhaa kumekuwa na mjadala kwamba Afrika haiwezi kuendelea kwa kutegemea misaada na zaidi utegemezi wa misaada umehusishwa na kuongezeka kwa umaskini wa Bara la Afrika.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu. (Picha na Maktaba).
Nikumbushe alichoandika mchumi nguli, Dambisa Moyo kwenye kitabu chake DEAD-AID, amesisitiza hoja hiyo katika ukurasa wa 11 ambapo ameonesha kuwa, wakati kiwango cha misaada kwa Bara la Afrika kilikuwa juu zaidi ( peak) katika miaka ya 1970s mpaka 1998, hicho ndio kipindi ambacho Afrika ilitoka kuwa na asilimia 11 ya masikini wote duniani mpaka asilimia 66.
Hata hivyo, wapinzani wa hoja kuwa misaada inaongeza umasikini wamejenga hoja yao katika misingi kuwa tatizo ni udhaifu wa Serikali za Afrika katika kupanga na kutekeleza matumizi ya fedha za misaada kutokana na rushwa, ufisadi, matumizi mabovu na zaidi kupangiwa matumizi na watoaji mikopo na misaada.
Zaidi, wapinzani wa hoja kwamba misaada ni sababu ya umasikini wanasisitiza hoja yao kwa kurejea mfano wa namna msaada wa Marekani chini ya mpango wake wa 'Marshal plan' wa $15bn ulivyofufua uchumi wa Ulaya baada ya vita ya II ya Dunia na kuhoji kwa nini Afrika inayopokea misaada takribani $50bn kwa mwaka lakn bado imezidi kuwa bara linalozidi kudidimia kwenye umasikini.
Kwamba Afrika kutoka kuwa Bara lenya asilimia 11 ya masikini wote duniani mwaka 1970s mpaka zaidi asilimia 70 ya masikini mwaka 2019,na inakadiriwa kuwa kufikia mwaka 2030, Afrika litakuwa bara lenye asilimia 87 ya masikini wote duniani..( Ripoti ya Taasisi ya Utafiti BROOKINGS, March 28, 2019).
Ni hoja yangu kwamba, kilichotokea kwenye msaada/mkopo nafuu kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa ( IMF) kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa UVIKO-19 kwa nchi za Afrika, kinathibitisha hoja ya kwa nini tatizo sio misaada bali wanaopewa misaada.
Kwamba, wakati mataifa mengi barani Afrika yametumia sehemu kubwa ya fedha za IMF za kupambana na ugonjwa wa UVIKO-19 kwa semina, warsha, kampeni, ununuzi wa vifaa tiba kukabili UVIKO-19 kwenye hospitali na vituo vya afya, makongamano ya uelimishaji na ununuzi wa shehena za barakoa kujikinga na ugonjwa huu, Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amefanya tofauti kwa lengo lile lile.
Ndio msingi wa hoja kwamba Rais Samia Suluhu Hassan amejenga hoja IMF na kukubalika kwamba kukabili UVIKO-19 Tanzania inahitaji kuongeza madawati na madarasa ili wanafunzi wasibanane darasani na hivyo kupunguza uwezekano wa wanafunzi kuambukizana UVIKO-19.
Kwa sababu hii Rais Samia Suluhu Hassan amefuta tatizo la madawati na madarasa kwa mwaka 2022 kwa kutenga sehemu ya fedha za IMF/ UVIKO-19 kukamilisha maboma ya madarasa 15,000 na madawati 462,795. Nguvu na muda ambao ungetumika kulitatua tatizo hili tutavitumia kushughulika na changamoto zingine.
Kwamba zinunuliwe gari 25 za kuchimba visima kila mkoa na mitambo mitano ya kuchimba mabwawa ili kupunguza tatizo la upatikanaji maji kama njia ya kukabili UVIKO-19.
Nakumbuka Ripoti ya Taasisi ya Tafiti za Maoni ( Opinion Survey) ya SYNOVATE ambayo ni ya 5 kwa ukubwa duniani, mwaka 2008 ilionesha kuwa maji ndio ilikuwa kero namba moja Tanzania.
Maji ni uhai, na Tafiti zinaonesha kwamba kwenye kila $1 inayowekezwa kwenye mradi wa maji inaokoa $4.2 ambazo zingetumika kutibu magonjwa yanayotokana na ukosefu maji safi na salama (WHO report , November 19, 2014).
Hivyo Rais Samia Suluhu Hassan anazitumia fedha za IMF/ UVIKO-19 kukabili tatizo la maji ambalo ni ajenda ya nchi hata kabla ya UVIKO-19.
Amelitumia tatizo la UVIKO-19 kukabili tatizo la upungufu wa magari ya kubeba wagonjwa kwa kununua gari hizo 395 zitakazosambazwa vituo vya Afya na Hospitali nchi nzima.
Na kwamba tuongeze vyuo vya VETA 32 ili kupunguza msongamano wa wanafunzi kuepuka kuambukizana UVIKO19.
Yote hii ni Rais Samia Suluhu Hassan anatekeleza ajenda ya Dira ya Taifa ya 2025 ya kuongeza nguvu kazi yenye ujuzi kiasi ( semi-skillied) kwa kutumia fedha za IMF/UVIKO-19.
Ni wazi kama Bara la Afrika lingekuwa na viongozi wenye fikra kama za Rais wetu Samia Suluhu Hassan kuhusu matumizi ya mikopo nafuu na misaada wana wa Afrika wangeona tofauti kubwa sana kwenye mataifa yao.
Ukisoma taarifa ya IMF ya Oktoba 08, 2021, kiasi cha $26.46bn au zaidi ya shilingi trilioni 60.86 kilichokwishatolewa cha kwa ajili ya kukabili UVIKO-19 kwenye nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambao ni ukanda masikini zaidi duniani kwa kwa ajili ya mpango wa kukabili UVIKO-19. Ni wazi kama nchi hizo zingekuwa na mfumo kama wa Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, ni wazi zingeacha alama kubwa sana ya maendeleo.
Lakini ndio hivyo, wengi zimeishia kuagiza barakoa na vifaa vya hospitali, semina, warsha na makongamano ya kujengeana uwezo wa namna ya kujikinga na UVIKO-19.
Wakati Tanzania imepata dola milioni 567 na Rais anakuja na mpango ambao sio tu wenye uwazi na tija kubwa kwenye uchumi wa nchi bali kwa uwazi wa kiwango cha juu hata kufanya watanzania kuona fahari ya mkopo husika.
Leo sitaki kuongelea kinachoendelea kwa jirani rafiki na jirani utaratibu wa fedha hizo za IMF/ UVIKO-19. Hadi siku nyingine.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA FUPI NI MKUU WA MKOA WA SIMIYU, MHESHIMIWA DAVID KAFULILA.