Na Robert Kalokola,Geita
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule amesema kuwa, Benki ya NMB imesaidia shughuli za mbio za Mwenge wa Uhuru kwa kutoa vifaa kwa vijana wa halaiki mia tano kwa ajili ya matumizi ya kilele cha mbio maalum za mwenge Oktoba 14, mwaka huu.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule akitazama moja ya vifaa kwa ajili ya shughuli za Mwenge vilivyotolewa na NMB, kushoto ni Meneja wa Kanda ya Ziwa, Baraka Radislaus. (Picha na Robert Kalokola/Diramakini Blog).
Amesema kuwa, vifaa hivyo ambavyo ni miavuli mia tano,truck suti mia tano zote kwa ajili ya vijana wa halaiki na shati 30 kwa ajili ya meza kuu ni nusu ya mahitaji ya mkoa ambayo ni vijana elfu moja watakaoshiriki kwenye sherehe za kuzima mwenge.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule ameagiza vifaa hivyo kusimamiwa kwa uadilifu mkubwa ili vitumike kwa malengo yaliyokusudiwa kwa ajili ya vijana hao.
Senyamule ameongeza kuwa licha vifaa hivyo kutumika katika shughuli ya kuzima mwenge Oktoba 14, mwaka huu pia vitatumika kuitangaza benki hiyo.
Amesema, benki hiyo inatoa ushirikiano mzuri kwa serikali kila wanapoishirikisha kwenye mipango na shughuli zake na kuongeza kuwa benki hiyo ni mbia mzuri wa serikali ambapo serikali inamilki zaidi ya asilimia 33 ya hisa.
Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa, Baraka Radislaus amesema kuwa, vifaa hivyo vina thamani ya shilingi milioni sabini (70).
Amesema, benki hiyo imetoa vifaa hivyo ili kuunga mkono Mkoa wa Geita katika shughuli za mbio za Mwenge.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule akipokea miamvuli kwa ajili ya vijana wa halaiki wa Mbio za Mwenge wa Uhuru iliyotolewa na NMB kushoto ni Meneja wa Kanda ya Ziwa, Baraka Radislaus. (Picha na Robert Kalokola/Diramakini Blog).
Radislaus ameongeza kuwa, benki hiyo imeamua kuunga mkono Mkoa wa Geita kwa kutoa vifaa hivyo ili kuboresha utendaji katika shughuli hasa kwenye kilele cha kuhitimisha mbio za Mwenge.
Meneja Radislaus ameongeza kuwa, mbali na kuchangia vifaa hivyo pia benki hiyo inashiki katika maonyesho ya Wiki ya Vijana yanayofanyika katika viwanja vya Mazaina wilayani Chato.
Amefafanua kuwa, huduma ambazo benki hiyo inatoa ni pamoja na kutoa ufafanuzi wa huduma mpya ya mkopo kwa wakulima kwa ajili ya kilimo.
Benki hiyo inatoa huduma ya mkopo mpya wa kilimo kwa riba nafuu wa asilimia kumi (10) tu kwa mkopaji ili kuweza kuwasaidia wakulima kuzalisha kwa tija na kujiongezea kipato.
Mwenge wa Uhuru ulipokelewa mkoani Geita Oktoba 9, mwaka huu na unaendelea na mbio zake katika wilaya zote tano za mkoa huo na mbio hizo zitahitimishwa Oktoba, 14 mwaka huu katika Wilaya ya Chato na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan.