Rhobi Samwelly ataja faida za wazazi na walezi mkoani Mara kuwapatia watoto wao elimu

NA FRESHA KINASA

Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania linalojishughulisha na mapambano ya ukatili wa kijinsia mkoani Mara, Rhobi Samwelly, amewaasa wazazi na walezi mkoani humo kuwa mstari wa mbele kuwezesha kuinua kiwango cha ufaulu wa kitaaluma kwa watoto wao ikiwemo kujitolea kwa hiari ujenzi wa miundombinu, kuchangia chakula shuleni ili watoto wao wasome kwa ufanisi pamoja na kufuatilia kwa karibu maendeleo yao ya kitaaluma kwa kushirikiana na walimu.
Mkurugenzi wa HGWT, Rhobi Samwelly akizungumza katika mahafali ya wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne Shule ya Sekondari Buhemba.
Skauti wa Buhemba sekondari wakitoa burudani.

Rhobi ameyasema hayo leo Oktoba 15, 2021 wakati akizungumza katika sherehe za mahafali ya 13 ya wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Buhemba iliyopo Wilaya ya Butiama, ambapo amesema kuwa mchango wa wazazi na walezi katika kuwezesha matokeo chanya kwa wanafunzi unahitajika sana, badala ya kuwaachia jukumu hilo Serikali na walimu peke yao. 

Na hivyo akasisitiza wawe sehemu muhimu ya kuchagiza ufanisi katika sekta ya elimu.

"Wazazi mshiriki vyema kusaidia kuchangia chakula kusudi wanafunzi wapate huduma ya chakula wakiwa shuleni, hii itasaidia sana waweze kusoma kwa ufanisi. Pia ni muhimu kwa wazazi na walezi kufuatilia maendeleo ya kitaalamu ya watoto hii itasaidia kujua maendeleo yao wakiwa shuleni na pia mjenge ukaribu na walimu sambamba na kuwapunguzia majukumu watoto wa kike wanapokuwa nyumbani ili wapate muda mwingi wa kujisomea,"amesema Rhobi.

Katika hatua nyingine, Rhobi amewaasa wazazi na walezi kuwapa fursa sawa ya elimu watoto wa kike sawa na watoto wa kiume kwani wana nafasi sawa ya kuleta mapinduzi ya kiuchumi na kijamii katika jamii na taifa pia badala ya kuwafanya kama kitega uchumi kwa kuwaoza na kujipatia mali. Akahimiza wawezeshwe kwa hali na mali ili watimize ndoto zao.
Pia, amewaasa wahitimu hao kwenda kuwa kielelezo bora katika jamii kwa kutojihusisha na tabia mbaya ambazo ni kinyume cha sheria za nchi hatua ambayo itawafanya wafikie malengo yao.

Kwa upande wake Mkuu wa Sekondari Buhemba, Emmauel Mpanduji amesema kukosekama kwa huduma ya chakula shuleni hupelekea baadhi ya wanafunzi kutoroka shuleni kwani wengi wao wanapokuwa za msingi hupatiwa chakula na Shirika la PCI na hivyo wanapofika sekondari hukosa huduma hiyo na hivyo mahudhurio darasani yanakuwa hafifu.

Pia, Emmanuel amesema kuwa, kukosekama kwa bweni shuleni hapo ni mojawapo Kati ya sababu ambazo zinachangia baadhi ya wanafunzi kutokufanya vizuri hasa wanaoishi mbali na shule hiyo na kwamba iwapo bweni litajengwa litasaidia kwa sehemu kubwa kuinua ufaulu wa taaluma shuleni hapo.
Awali akisoma risala ya wahitimu hao, Agatha Joseph amesema kuwa shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 550 Kati yao wavulana ni 281, wasichana 269. Huku Wahitimu akisema walianza kidato cha kwanza wakiwa 188 kati yao wavulana wakiwa ni 99 wasichana 89 lakini kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utoro, mimba, kuhama, kufeli kwenye mitihani ya kidato cha nne wameweza kuhitimu wanafunzi 79 wavulana wakiwa 44 na wasichana 35.

Ameongeza kuwa, wakiwa shuleni hapo wameweza kujifunza masomo ya sekondari, kuwa na klabu ya fema ambayo inajumuisha utoaji wa elimu ya kijinsia, kujifunza utunzaji wa Mazingira, kujifunza nidhamu na utii, pamoja na kuanzisha klabu ya Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania kujifunza madhara mbalimbali ya Ukatili wa Kijinsia na kutoa elimu hiyo kwa wengine.

Amesema shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo hostel, upungufu wa vyumba 9 vya madarasa na maabara, upungufu wa vitabu vya masomo ya Sanaa, maktaba ya kutunzia vitabu, kompyuta, upungufu wa vifaa vya kuandalia mitihani akaomba zipatiwe ufumbuzi kwa lengo la kuimarisha ufanisi wa taaluma shuleni hapo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news