NA FRESHA KINASA
Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania linalojishughulisha na mapambano ya ukatili wa kijinsia mkoani Mara, Rhobi Samwelly amesema watoto wa kike wana nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii na taifa kwa ujumla, hivyo wazazi na walezi wawape fursa ya kusoma na kuwawekea mazingira wezeshi ili watimize ndoto zao.
Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, Rhobi Samwelly akikabidhi cheti kwa mmoja wa Wahitimu wa kidato Cha nne katika Shule ya Sekondari Mwembeni kulia kwake ni Mkuu wa shule hiyo Joseph John.
Rhobi ameyasema hayo Oktoba 22,2021alipokuwa mgeni rasmi katika Mahafali ya 29 ya Wahitimu wa Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Mwembeni iliyopo Manispaa ya Musoma Mkoa wa Mara. Ambapo pamoja na mambo mengine amesema, iwapo wazazi na walezi wataweka msukumo chanya wa kuwasomesha watoto wa kike jamii na taifa litazidi kusonga mbele katika nyanja za maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
"Niwaombe wazazi na walezi tuwape fursa ya elimu watoto wa kike kusudi wasome kama ilivyo kwa watoto wa kiume, tumeona katika Taifa letu viongozi wengi wanawake wanafanya vizuri sana katika nyadhifa mbalimbali za uongozi. Wapo Mawaziri, Wakuu wa mikoa, Wakuu wa taasisi mbalimbali, wakurugenzi na kipekee kabisa Rais wetu Samia Suluhu Hassan ambaye ni kiongozi shupavu na mzalendo ambaye kwa sasa analeta maendeleo katika nchi yetu,"amesema Rhobi.
Ameongeza kuwa, zipo baadhi ya changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili watoto wa kike ikiwemo baadhi ya jamii kuwafanya kama chanzo cha kipato na hivyo kutowapa kipaumbele kuwasomesha, jambo ambalo halifai hata kidogo, na hivyo amesisitiza kila mmoja kushiriki kikamilifu kutatua changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili sambamba na kuwapatia mahitaji yao ya Msingi na kuwapunguzia muda wa Majukumu wanapokuwa nyumbani ili kupata muda wa kujisomea.
Aidha, Rhobi amewataka wahitimu hao kujitambua na kuhakikisha kwamba, wanakuwa na ndoto na wajitume kuzitimiza, huku pia akiwaomba watumie muda vizuri watakapokuwa nyumbani kwa kufanya mambo ya uzalishaji, kutii wazazi na watu wote na pia wajiepushe na marafiki wabaya watakaokwamisha malengo yao na kuwaingiza katika vitendo viovu.
Akisoma taarifa ya Shule Makamu Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Labanus Masinde Manyama amesema kuwa, shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 624 ambapo wanafunzi wa kike ni 266 na wa kiume ni 358, huku wahitimu akisema ni 148 kati yao wanafunzi wa kike ni 72 na wanafunzi wa kiume ni 76 ambapo amesema wakiwa shuleni hapo wameweza kupikwa kitaaluma, kiroho na kijamii.
Ameongeza kuwa, shule hiyo imekuwa ikifanya mikakati mbalimbali ya kuinua taaluma ikiwemo kuwajengea wahitimu kujiamini kupitia mitihani ya kila mwezi, nusu muhula, jimbo, mazoezi ya mara kwa mara, uwepo wa walimu wa kutosha wa masomo yote, kumaliza syllabus mapema na kurudia, kusimamia nidhamu ya wanafunzi, matumizi ya lugha ya kiingereza muda wote, programu maalumu kwa wanafunzi wote pamoja na kusimamia maandalizi ya walimu kabla ya kuingia darasani kufundisha.
"Katika mitihani ya miaka mitatu iliyopita kwa upande wa kidato cha sita mwaka 2019 daraja la kwanza walikuwa wanafunzi 14, daraja la pili 45, daraja la tatu 13 daraja la nne 0. Mwaka 2020 daraja la kwanza 3, daraja la pili 49, daraja la tatu 29 daraja la nne 0. Mwaka 2021 daraja la kwanza wanafunzi 13, daraja la pili 31, daraja la tatu 13, daraja la nne 0,"amesema.
Upande wa kidato cha nne amesema mwaka 2018 daraja la kwanza wanafunzi 5,daraja la pili 40, daraja la tatu51 na daraja la nne 0. Mwaka 2019 daraja la kwanza 12, daraja la pili 51, daraja la tatu 62, daraja la tatu wanafunzi 35, na daraja la nne 0. Huku mwaka 2020 daraja la kwanza 19, daraja la pili 58, daraja la tatu 55, daraja la nne 35 na daraja O hakuna.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hiyo Dakt. Muniko amewashauri Wahitimu hao kutunza afya zao ikiwemo kujiepusha na matendo mabaya yanayoweza kuwapelekea kupata magonjwa ya kuambukiza, kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya, makundi mabaya akawasihi watambue afya ni Msingi wa kufikia malengo yao.
Akisoma Risala ya Wahitimu hao Latifa Haji amesema kuwa kuwepo kwa Hostel shuleni hapo kumesaidia kupunguza ushawishi kwa wanafunzi wa kike na hivyo kusoma vizuri, huku akitoa mapendelezo ya kuanzishwa mashindano ya kitaaluma ili kuwaandaa vyema wanafunzi katika mitihani yao mbalimbali pamoja na kuanzisha Zahanati kwa lengo la kuwahudumia wanafunzi.