Na Doreen Aloyce,Diramakini Blog
KATIBU wa NEC Itikadi na Uenezi Chama cha Mapinduzi (CCM), Shaka Hamdu Shaka amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kupokea mkopo wenye masharti nafuu wa dola milioni 579 sawa na sh.trilioni 1.3 za Kitanzania kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya mipango ya kimaendeleo kwa kipindi cha miezi tisa, fedha ambazo zimetolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).
Sambamba na hilo amewataka viongozi wa kamati za siasa za chama hizo kuanzia ngazi ya shina hadi mkoa kusimamima matumizi ya fedha hizo kikamilifu na ziende kutumika kama ilivyokusudiwa.
Akiongea leo na waandishi wa habari jijini hapa, Katibu huyo amesema Rais Samia ameendelea kulinda tunu za taifa huku akihakikisha maendeleo endelevu yanapatikana kwa serikali na hata kwa mtu mmoja mmoja.
Shaka amesema, mkopo huo ni fursa muhimu kwa watanzania kwani mkopo huo umepatikana bajeti ya serikali ikiwa imepita hivyo hakuna litakalotetereka kutokana na kupata kwa mkopo huo.
"Tukumbuke kwamba fedha hizi sio sadaka ni fedha kwa ajili ya maendeleo ya watanzania ambapo zikitumika vizuri uchumi wa nchi utakuwa zaidi na hata wananchi mmoja mmoja wanakwenda kunufaika,hivyo basi chama kinaomba kuendelea kumuunga mkono Rais wetu kwani ameonekana kuwa na mapenzi mema kwa nchi na wananchi wake kwa ujumla ,"amesema Katibu huyo Shaka.
Katika hatua nyingine amewapongeza na kuwashukuru wananchi na wanachama wa wa Jimbo la Ushetu Mkoa wa Shinyanga kwa kukipa ushindi wa kishindo pamoja na jimbo la Konde Zanzibar.