NA GODFREY NNKO
Hatimaye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefufua matumaini ya kufuzu kwenye Fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Qatar.
Ni baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Benin jioni ya leo katika dimba la L' Amitié mjini Cotonou, Benin.
Taifa Stars imepata bao pekee kupitia mshambuliaji wa Wydad Athletics ya Morocco, Simon Happygod Msuva.
Bao ambalo limepatikana ndani ya dakika ya sita tu, akimchambua kipa Owalabi Franck Saturnin wa Valenciennes Ligue 2 ya Ufaransa baada ya kuwatoka mabeki wa Benin kufuatia kuanzishiwa mpira wa kurusha upande wa kulia wa Uwanja.
Aidha, Taifa Stars inayofundishwa na kocha Mdenmark, Kim Poulsen inafikisha alama saba, sawa na Benin baada ya mechi tatu wakiwa mbele ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) yenye alama tano na Madagascar ambayo haina alama baada ya mechi tatu.
Kutokana na ushindi huo mkubwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amewapongeza.
"Nimefurahishwa na ushindi wa Taifa Stars wa 1-0 dhidi ya Benin. Nawapongeza wachezaji, benchi la ufundi na TFF, kwa jitihada za kushinda pambano la leo.
"Nawatakia kheri katika michezo iliyobaki ili Tanzania iweze kufuzu kucheza Kombe la Dunia nchini Qatar mwakani,"amesema Rais Samia.
Tags
Michezo