NA DOREEN ALOYCE
Mkuu wa ofisi ndogo ya Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Neema Nima Sitta amesema jumla ya tani 17,000 ya zao la mtama zimeuzwa katika nchi ya Sudan Kusini jambo ambalo limesaidia kuinua soko la zao hilo nchini.
Sitta ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na vyombo vya habari juu ya zao la mtama na kudai kwamba zaidi ya shilingi bilioni tisa kwa miaka miwili zimepatikana kupitia zao hilo.
Amesema kuwa, zaidi ya wakulima 22,000 wa wilaya tano za Mkoa wa Dodoma wameunganishwa kwa wanunuzi wa mtama Sudan Kusini kupitia WFP ambapo soko la zao hilo ni kubwa.
Akitaja wakulima ambao wameanza kunufaika na kilimo hicho ambacho ni himilivu kupitia mpango huo unaoendeshwa kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania ni wilaya za Dodoma,Kondoa,Chemba, Mpwapwa,Bahi na Dodoma Mjini.
"Hili zao la mtama limekuwa na soko kubwa katika nchi ya Sudan Kusini na WFP inaendesha programu maalumu ya kulima zao hilo katika vijiji zaidi ya 200 kwenye wilaya za Mkoa wa Dodoma ambapo shirika linawatafutia soko wakulima kwa mashirika binafsi katika nchi hiyo ikiwa ni sehemu ya wanunuzi kwa ajili ya kambi za wakimbizi,"amesema Sitta.
Aidha, amesema katika mradi huo ambao wanashirikiana na Serikali wameanza vijiji 203 katika Mkoa wa Dodoma na lengo ni kupanua mradi huo kwani kuna mahitaji makubwa ya mtama Sudan Kusini na kwamba kilimo cha Mtama unalimwa kwa mfumo wa kilimo hai na pia kuondoa matumizi ya mbolea za viwandani na dawa.
"WFP tukiwa tunashirikiana na Serikali tunajivunia mradi huu umekuwa na mafanikio ila tumegundua zao hili limekuwa na mahitaji makubwa kwa nchi ya Sudan Kusini na kutokana na uhitaji huu mkubwa kwenye soko, sisi WFP tunafikiria kupanua mradi huo na kufikisha kwenye wilaya nyingi na mikoa mingine Tanzania,"amesema Sitta.