NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, zahanati ya Kijiji cha Isowezy kilichopo Kata ya Isansa wilayani Mbozi mkoani Songwe ilikuwa ikijengwa kwa zaidi ya miaka 20 bila kukamilika.
Wanakijiji kwa nyakati tofauti, wameieleza DIRAMAKINI BLOG kuwa, zahanati hiyo kila ilipokuwa inajengwa ilikuwa inabomoka katika mazingira ya kutatanisha.
Aidha, wengi wamehusisha hali hiyo na imani za kishirikina ambapo jitihada za makusudi zimechukuliwa hadi kuikamilisha ili ianze kutoa huduma kwa wananchi na iliwahi kubomoka mara tatu, hivyo wengi kususia kushiriki katika ujenzi.
Omari Mgumba ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Songwe ametembelea zahanati hiyo na kuizindua rasmi.
Mheshimiwa Mgumba ameelezwa kuwa, ujenzi wake umekamilika hivi karibuni na sasa inatarajia kuanza kutoa huduma za afya kwa wananchi.
Rehema Simbeye ambaye ni Afisa Mtendaji wa Kijiji alimweleza Mkuu wa Mkoa kuwa, zahanati hiyo ilianza kujengwa kwa nguvu za wananchi tangu mwaka 1993.
Amesema kuwa, hadi kukamilika kwa ujenzi wa zahanati hiyo, gharama iliyotunika ni kiasi cha shilingi milioni 69,246,000.
Simbeye ameongeza kuwa, nguvu ya wananchi iliyotumika ni sawa na shilingi 16,446,000 na Serikali Kuu ikatoa shilingi milioni 50, huku wadau wengine wakichangia vifaa mbalimbali.