NA MWANDISHI MAALUM
Wafungwa 69 ambao wamehukumiwa adhabu ya kunyongwa, wamemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan awapunguzie adhabu ya kunyongwa na kuwapatia adhabu mbadala.
Makatibu wakuu Sifuni Mchome, John Jingu na Christopher Kadio wakiwa nje ya Gereza Kuu la Uyui lililopo mkoani Tabora mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo yao na viongozi wa Gereza, wafungwa na mahabusu. Katika mazungumzo hayo na na mahabusu na wafungwa waliohukumiwa kunyongwa wamemuomba Rais Samia awaonee huruma. (Na Mpigapicha Wetu).
Wafungwa hao ambao wapo katika Gereza Kuu la Uyui mkoani Tabora, wametoa ombi lao hilo kupitia risala yao waliyoisoma mbele ya Makatibu wakuu watatu wakiongozwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa Sifuni Mchome waliofika gerezani hapo kuzungumza na Uongozi wa Gereza, mahabusu na wafungwa.
Akisoma risala hiyo kwa niaba ya wafungwa wenzake waliohukumiwa kunyongwa, mfungwa kiongozi No 143/2012 Masali Misalaba, wafungwa hao wamesema, wanaomba huruma ya Mheshimiwa Rais Samia awabadilishie adhabu hiyo na kupewa adhabu mbadala ili nao waweze kufanya kazi kama ilivyo kwa wafungwa wengine.
“Mheshimiwa Katibu Mkuu wa Katiba na Sheria, kwanza, tunashukuru sana kwa kututembelea wewe na ujumbe wako, sisi wafungwa ambao tumehukumiwa kunyongwa, tunakuomba utufikishie ombi letu kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan atuonee huruma na atupunguzie adhabu hii ili nasi tuweze kufanya kazi, kwa kweli tunawakati mgumu na tunawasumbua sana askari magereza tunaomba sana utufikishie ombi letu kwa Mheshimiwa Rais,"amesema Mfungwa Kiongozi kwa niaba ya wenzake.
Wafungwa hao ambao wamehukuhimiwa kunyongwa hadi kufa, walipewa nafasi na uongozi wa Gereza Kuu la Uyui kujumuika na mahabusu na wafungwa wenzao katika kikao hicho ambacho walipata fursa ya kuelezea changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Wafungwa hao waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa walikuwa wamevalia sare yao ya rangi ya blue, wenye umri tofauti wengine ni wazee ambao walisaidiwa kutembea na wafungwa wenzao, wengine wlionekana wamevaa rosali zao shingoni au wameshika tasbihi mikononi, wengine hata walikuwa na biblia, walikuwa ni wasafi na nyuso zenye matumaini licha ya kwamba walikuwa wamehukumiwa adhabu ya kifo.
Pamoja na wafungwa waliohukumiwa kunyongwa kuomba huruma ya Rais. Mahabusu na wafungwa wengine nao walitoa yao ya moyoni mbele ya Makatibu Wakuu hao ambao ni nadara sana kutokea kwamba Makatibu Wakuu watatu kutoka Wizara Tofauti lakini majukumu yao yanaingiliana katika masuala ya utoaji haki jinai na haki madai wakawa na ziara ya pamoja.
Katika risala yao, iliyosomwa kwa niaba yao na Mfungwa Enock Ezekiel Kakamba, wameiomba serikali kuangalia upya utaratibu wa msamaha wa wafungwa unaotolewa na Rais.
Wamependekeza kwamba wigo wa msamaha unaotolewa na Rais upanuliwe zaidi na kuwahusisha pia wafungwa ambao wametumiki vifungo virefu vya zaidi ya miaka kumi.
“Mheshimiwa Katibu Mkuu, tunaomba kwamba, msamaha wa Rais ikiwezekana uhusishe pia wafungwa ambao wameshatumikia vifungo vyao kwa zaidi ya miaka kumi na kuonyesha tabia njema, tunaomba hivi kwa sababu msamaha ambao umekuwa ukitolewa kwa wafungwa ambao hawajatumikia vifungo vyao kwa muda mrefu, wakishaachiwa baada ya muda mfupi wanarejea tena magerezani kwa sababu muda waliokaa wanakuwa hawajajifunza chochote tofauti na mfungwa ambaye ametumikia zaidi ya miaka 10 huyu akipata msamaha hawezi tena kurudi kwenye uhalifu kwa sababu tayari ameshajifunza na hatatamani kurudi tena gerezani,”amesema.
Vile vile mahabusu hao wameomba kushughulikiwa kwa suala la uchelewesheaji wa upelelezi, uchelewaji wa kutolewa kwa nakala ya hukumu kwa wakati, uchache wa viakao maalaum vya mahakama kuu na mahakama ya rufani hasa kwa kesi za mauaji na kesi za uhujumu uchumi.
Pia wafungwa na mahabusu wao wameomba sheria ya Parole inagaliwe upya ili iweze kuwa na wigo mpana tofauti na ulivyo hivi sasa ambapo ina wigo mfinyu katika makosa na muda. Kutokana na kwamba ni makosa machache sana yanayokubalika wa parole na muda wa kuwa na sifa ya kupendekezwa kwenye Parole ni mrefu sana ambao ni 1/3 ya kifungo.
Akijibu ombi la wafungwa waliohukumiwa kunyongwa, Katibu Mkuu, Profesa Mchome, amesema atalifikisha ombi hilo kwa mamlaka zinazohusika.
Kabla ya kuzungumza na mahabusu na wafungwa, Makatibu wakuu hao pamoja na ujumbe walioongoza nao walipata fursa ya kuonja au kula chakula ambacho kilikuwa kimeandaliwa kwaajili ya mahababusu na wafungwa .
Kwa mujibu wa Mkuu wa Gereza Kuu la Uyui ACP Mussa Said Mkisi, Gereza la Uyui ambalo limejengwa mwaka 1946 linauwezo wa kupokea wafungwa na mahabusu wa kiume kutoka mikoa ya jirani, na vile vile kupokea wafungwa kutoka Magereza Makuu kama vile Butimba – Mwanza, Isanga- Dodoma, Maweni-Tanga na Ukonga Dare es Salaam
Hadi wakati Makatibu Wakuu hao wanatembelea Gereza hilo, kulikuwa na wafungwa na mahabusu 767. Idadi hiyo ikijumuisha wahalifu ambao si raia wa Tanzania kutoka nchi za Burundi, Kongo ( DRC) na Ethiopia.
Mkuu wa Gereza hilo ACP Mussa Saidi Mkisi amewaambia Makatibu wakuu hao ingawa msongamano wa wafungwa na mahabusu katika Gereza hilo ni wawastani, lakini changamoto hiyo bado kutokana na ongezeko la watu na uhalifu nchini licha ya kwamba Mahakama imekuwa ikijitahidi kusikiliza kesi za mahabusu na wafungwa.
“ Gereza lina msongano wa wastani wa wahalifu kwani hadu leo ( jumatatu) tunao wahalifu 767 wakati uwezo wa Gereza ni kuhifadhi wafungwa na mahabusu 650 ziada ni wahalifu 117 sawa na asilimia 18” akaeleza Mkuu wa Gereza ACP Mussa Saidi Mkisi.
Katika taarifa yake, Mkuu wa Magereza alielezea changamoto nyingine kuwa ni ukosefu wa magodoro na mablanketi kwa ajili ya mahabusu na wafungwa, uchache wa maafisa na askari magereza. Na wadau wa hakijinai na baadhi ya wananchi kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu adhabu mbadala.
Makatibu Wakuu Profesa Sifuni Mchome, ( Wizara ya Katiba na Sheria) John Jingu( Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto) na Christopher Kadio ( Mambo ya Ndani) wapo katika ziara ya kujifunza na kufanya tathimini kuhusu mnyororo wa utoaji haki jinai na haki madai katika mikoa ya Tabora, Kigoma na Kagera.
Wakiwa mkoani Tabora pamoja na kutembelea Gereza Kuu la Uyui lakini pia wamekuwa na vikao mbalimbali na wadau wanaohusika na suala zima la utoaji haki, wakiwamo Mahakama, Magereza, Polisi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka na Ustawi wa Jamii.