Wananchi Bumbuli wachangamkia chanjo ya UVIKO-19

Na Yusuph Mussa, Bumbuli

ZOEZI la chanjo katika Halmashauri ya Bumbuli, Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga limefanikiwa kwa zaidi ya asilimia 99 baada ya hadi Oktoba 9, 2021 wananchi 1,423 kuchanja chanjo ya UVIKO-19.

Jitihada za makusudi zilifanyika katika kuwapa elimu wananchi kuhusu kupata chanjo hiyo ili kujikinga na maradhi ya UVIKO 19, ambapo timu ya wataalamu wa afya wa halmashauri hiyo waliweza kufika kwenye maeneo ya ibada kama kanisani, sokoni, kwenye magulio, hotelini hadi nyumba kwa nyumba.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Oktoba 10, 2021, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli Dkt. Idd Msuya, alisema zoezi hilo limekamilka, na wanatarajia kutoa taarifa rasmi Oktoba 11, 2021 kuhusu zoezi hilo namna lilivyokwenda na mafanikio yake. 

"Tumefanya jitihaza za kila namna kuona wananchi wanamuelewa Rais wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan na dhamira yake ya dhati ya kupambana na ugonjwa huu wa UVIKO 19. Hadi Oktoba 9, 2021, tumechanja wananchi 1,423. Tunaamini malengo yetu yametimia, lakini taarifa rasmi ya zoezi la chanjo tutalitoa kesho (leo)" alisema Dkt. Msuya.

Katika kufanikisha zoezi hilo, timu ya wataalamu wa afya wa Halmashauri ya Bumbuli walifika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Usharika wa Ngwelo B katika Kijiji cha Msamaka, ambapo Kiongozi wa Kanisa hilo Richard Sekidolima aliwakaribisha mbele ya kanisa hilo na kuanza kutoa somo juu ugonjwa wa UVIKO 19.

Ambapo Dkt. Ambwene Mwakyusa na Mlongeni Njemeti ambaye ni Mfamasia, walitoa somo kuhusu ugonjwa wa UVIKO 19 na chanjo ya Jensen inavyoweza kumsaidia mtu asiweze kupata madhara makubwa pindi akipata maambukizi, na waumini walielewa umuhimu wa chanjo na 14 kati yao wakachanja nje ya kanisa hilo wakiongozwa na Mwalimu Msaidizi wa Kanisa hilo Joseph Sekidolima.

Mratibu wa Chanjo hiyo katika Halmashauri ya Bumbuli Elizabeth Nyaki alisema wanafanya majumuisho ya mwisho, kwani kwao ni kama chanjo imekwisha, kwani walipewa chanjo 2,400, lakini katikati ya zoezi la kuchanja, kuna chanjo nyingine waliigawa kwa halmashauri nyingine mkoani Tanga ambayo ilikuwa na uhitaji mkubwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news