Washauri makosa ya kujifanya Afisa TAKUKURU, rushwa ya ngono yaondolewe katika makosa ya Uhujumu Uchumi

Na Mwandishi Maalum- Kigoma

Wajumbe wa Jukwaa la Haki Jinai Mkoa wa Kigoma, wameishauri Serikali, kuifanyia marekebisho Sura ya 329 marejeo ya mwaka 2019 ili kuondoa baadhi ya makosa kuwa ya uhujumu au kuhitaji kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka kufungua kesi.

Ushauri huo umetolewa siku ya Jumatano na Wajumbe hao wakati wa Kikao Kazi kilichoongozwa na Profesa Sifuni Mchome , Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria. Kikao hicho pia kiliwashirikisha Makatibu Wakuu, John Njingu, Katibu Mkuu Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, na Christopher Kidau, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani. Mwenyekiti wa Jukwaa la Haki Jinai Mwendesha Mashtaka Mkoa wa Kigoma, Riziki Matitu akiwasilisha Taarifa ya Jukwaa wakati wa Mkutano wa Kikao Kazi kilichoongozwa na Profesa Sifuni Mchome Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, wengine katika picha ni wajumbe wa Jukwaa hilo.

Makatibu hao watatu wapo katika ziara ya kikazi ya kutathimini utoaji wa hakijinai , mafanikio, changamoto na hata kuzitolea ufumbuzi au uamuzi wa papo kwa papo wa baadhi ya changamoto hizo.

Akiwasilisha Taarifa ya Jukwaa hilo kwa Makatibu Wakuu hao, Mwenyekiti wa Jukwaa, Mwendesha Mashtaka Mkoa wa Kigoma Riziki Matitu, ameyataja baadhi ya makosa ambayo yanahesabiwa kama uhujumu uchumi ni pamoja mtu kujifanya Afisa Takukuru na rushwa ya ngono.

“ Tunashauri na kupendekeza kwamba, Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 marejeo ya mwaka 2019, irekebishwe ili kuondoa baadhi ya makosa kuwa ya uhujumu uchumi na au kuhitaji kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka ili kufungua Kesi. Kwa mfano kosa la kujifanya Afisa Takukuru Kifungu cha 36 na rushwa ya ngono kifungu cha 25” akasema Mwenyekiti wa Jukwaa. Riziki Matitu.

Pamoja na kutaka kufanyiwa marekebisho kwa sheria hiyo, Jukwaa la Haki Jinai ambao wajumbe wake ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Mkuu wa Usalama wa Taifa wa Mkoa, Mkuu wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa, Mkuu wa Magereza, Mratibu wa Huduma za Kijamii na Mwenyekiti wa Bodi ya Msamaha Mkoa, limeshauri pia Sheria ya kulinda mashahidi na watoa taarifa Na 20 ya mwaka 2015 itengenezewe kanuni.

Jukwaa hilo linataka kutungwa kwa kanuni hizo kwa kile walichosema kumekuwapo na changamoto kubwa zinazowakabili mashahidi na watoa taarifa ikiwamo kutishiwa maisha au kutojitokeza kutoa ushahidi kwa kuhofia maisha yao na hata kuugeuka ushahidi waliokwisha kuutoa kutokana na vitisho wanavyopewa.

“Mhe. Katibu Mkuu sisi Jukwa la Haki Jinai, tunapendekeza pia Sheria ya kulinda mashahidi na watoa taarifa Na 20 ya mwaka 2013 itengenezewe kanuni kama ilivyoainishwa kwenye kifungu cha 15 cha sheria hiyo ili kuelekeza jinsi ya kutoa ulinzi kwa mashahidi au watoa taarifa wanaopata madhira kwa kushirikiana na vyombo vya uchunguzi au mashtaka”

Katika kupunguza msongamano wa mahabusu na wafungwa katika magereza, Wajumbe wa Jukwaa pia wameshauri haja na umuhimu wa matumizi wa adhabu mbadala kwa baadhi ya makosa na wakataka elimu zaidi itolewa kwa Mahakimu, Waendesha Mashtaka, Mawakili na Jamii ili iwe tayari kupokea adhabu hiyo bila kujenga viashiria vya rushwa ndani yake.

Wakatoa mfano kwamba, katika tathmini iliyofanywa mwezi Machi Mwaka huu na Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, iligundua kwamba kati ya washtakiwa 182 waliofungwa gerezani kifungo kisichozidi miaka mitatu ambao wangeweza kupewa adhabu ya huduma kwa jamii na hivyo ingesaidia sana kupunguza msongamano magerezani.
Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa Sifuni Mchome akizungumza katika kikao kazi kilichowahusisha Jukwaa la Haki Jinai Mkoa wa Kigoma na Jukwaa la kupinga ukatili wa Kijinsia uliofanyika siku ya Jumatano Mkoani Kigoma, wengine katika picha ni Katibu Mkuu Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto John Jingu na Chritopher Kidau, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani.

Hata hivyo jukwa hilo limesema adhabu za fine na huduma za jamii zipewe kipaumbele, isipokuwa uhalifu wa kutumia nguvu, unyanyanyi, uhaini, ugaidi na mauaji” wakasema wajumbe wa Jukwaa.

Akijibu mapendekezo nayo na mengine yaliyowasilishwa katika Kikao Kazi hiyo, Katibu Mkuu Profesa Sifuni Mchome, amesema.“ Katika hili la sheria ya TAKUKURU nisema tu mchakato wa mapitio ya sheria hiyo unaendelea vizuri, kwa sababu kuna baadhi ya makosa yasingekuwa na hoja ya kuwa katika sheria hii. Kuna baadhi ya makosa yakiwamo kwa mfano ni mali au fedha ya thamani gani inapashwa kuingia katika kosa la uhujumu uchumi, na mengine mengi tunayaangalia, si muda mrefu kazi hii itakuwa imekamilika” akabainisha Katibu Mkuu Mchome.

Kuhusu kutungwa kwa kanuni za kuwalinda mashahidi na watoa taarifa, Katibu Mkuu mchome amewahakikishia wadau hao wa Hakijinai kwamba kanuni hizo zitakuwa zimekamilika ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Aidha Katibu Mkuu Mchome amesema, Mamlaka ya Mwendesha Mashtaka sasa yameshushwa katika ngazi ya Mkoa na Wilaya kwa baadhi ya mashauri ili kupunguza uchelewesaji wa mashauri. Akasisitiza haja na umuhimu wa Taasisi zote zinazohusika na utoahi haki kufanya kazi kwa ushirikiano huku zijichukua tahadhari ya kutoingilia wajibu na mamlaka ya Taasisi nyingine.

Kuhusu wafungwa kukosa sifa za udhamini, Profesa Mchome amebainisha kwamba kazi imeaanza ya kufanyika kuhuisha mfumo wa Polisi, NIDA na Mahakama ili kurahisisha upatikanaji wa dhamana kwa watuhumiwa ambao makosa yao yanastahili dhamana.

Wakiwa Mkoani Kigoma, Makatibu Wakuu hao pia wamekuwa na mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Tobias Andegenye, Vikao Kazi na Wajumbe wa Kamati ya MTAKUWA ya Manispaa ya Kigoma/ Ujiji,Wajumbe wa Jukwaa la Uwezeshaji wa Wanawake Kiuchumi na pia walitembelea Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Gereza la Kigoma Mjini ( Bangwe) na Kambi ya Wazee Kibirizi.

Wakiwa katika Gereza la Bangwe, Makatibu Wakuu hao walitoa fursa kwa wafungwa na mahabusu kutoa kero zao.

Baadhi ya kero zilizowasilishwa na mahabusu na wafungwa hao ni pamoja na kutokuwa na bima ya afya na hivyo kuiomba serikali kuwafikiria.

Aidha wafungwa hao wameomba kupatiwa mablanketi na magodoro.

Gereza la Bangwe ambalo limejengwa mwaka 1938 likiwa na uwezo wa kuchukua wafungwa 69 sasa linauwezo wa kuhudumia wafungwa na mahabusu 198 baada ya kupanuliwa na kwamba halina msongamano.

Kwa upande wa huduma za Afya, Wafungwa 71 wamechanjwa kwa hiari chango ya Covid- 19 huku maafisa na askari 6 wamechanjwa kwa hiari yao. Makatibu Wakuu hao Ijumaa watakuwa Mkoani wa Kagera.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news