Wasiojulikana wavunja ofisi ya CHADEMA, wachoma nyaraka

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Watu wasiojulikana wamevunja ofisi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Tunduma na kuteketeza kwa moto nyaraka mbalimbali muhimu zilizokuwa ndani ya ofisi hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Janeth Magomi amesema, wamepokea taarifa za tukio hilo baada ya kupigiwa simu alfajiri na Katibu wa Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA) wa chama hicho Wilaya ya Momba, Mussa Mwaipata.

Magomi amesema kuwa,Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto walipofika eneo la tukio walibaini ofisi hiyo kuvunjwa na kuchomwa moto kwa nyaraka mbalimbali muhimu za ofisi hiyo.

Amesema, "baada ya kufika katika eneo la tukio tukiwa na wenzetu wa Zimamoto tulichokuta kimechomwa ni nyaraka mbalimbali muhimu na mbinu iliyotumika ni kuvunja mlango na kuingia ndani na kwenda moja kwa moja kwenye nyaraka na kuzichoma moto,”.

Ametaja vitu vingine vilivyochomwa moto kwenye tukio hilo ni furushi la nguo ambazo zilikuwa pembezoni mwa mlango uliovunjwa katika ofisi hizo.

“Pale nje mlangoni tuliona kuna furushi la nguo ambazo nazo zilichomwa moto,”amesema.

Kamanda Magomi amewaomba wananchi wenye taarifa yeyote muhimu kuhusu tukio hilo wazitoe kwa jeshi hilo ili wote waliohusika na tukio hilo la uvunjfu wa amani wakamatwe.

“Wakati sisi tukiendelea na uchunguzi wa kiintelejensia ili kuwafahamu au kuwabaini wote waliohusika, tunaomba mwananchi yeyote mwenye taarifa aje atupatie ili wahusika wote wapatikane kwa kuwa tukio hili halikubaliki hata kidogo,”amesema.

Kamanda Magomi amesema, hadi kufikia sasa hakuna mtu yeyote aliyekamatwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news