Wazee watoa adhabu kwa watumishi Mamlaka ya Maji, watakiwa kutoa ng'ombe dume watatu watakaochinjwa uwanjani

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Wazee katika vijiji vya Ayalagaya, Haysam na Gajal wilayani Babati mkoani Manyara kwa kauli moja wameridhia kuwa, watumishi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira mjini Babati (BAWASA) walipe faini ya ng'ombe dume watatu baada ya kuharibu chanzo cha maji katika mto Endalo na kusababisha taharuki kwa wananchi.
Akiongea kwa niaba ya wazee walioshiriki mkutano na mkuu wa mkoa wa Manyara, Makongoro Nyerere, mzee Michael Tsaghara ameuambia mkutano kuwa, mafundi wameomba msamaha, hivyo wazee wamesema msamaha utakubalika endapo watalipa faini ya kulipa madume watatu wa ng’ombe watakaochinjwa na kuliwa hapo kwenye uwanja wa mikutano.

Mafundi hao wakiongozwa na Mhandisi Rashidi Cherehani waliridhia kulipa faini hiyo na tayari wako sokoni wakiwasaka madume hao watatu watakaowasilishwa uwanjani tayari kwa kitoweo cha wazee wa kata nzima na majirani zao.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya maelezo ya pande mbili kutolewa mbele ya mkuu wa mkoa huo na kuonekana mafundi wa BAWASA walikuwa wakifanya shughuli zao bila kuwashirikisha viongozi wa kata husika ya Ayalagaya.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Makongoro Nyerere alifanya ziara rasmi ya kufanya upatanisho kati ya viongozi wa BAWASA na wakazi wa vijiji vya Ayalagaya, Haysam na Gajal kwa madai ya mafundi wa taasisi hiyo kuharibu chanzo cha maji katika mto Endalo na kusababisha maji kukosekana kwa siku saba.

Akitoa maelezo mbele ya mkuu wa mkoa, Diwani wa Kata ya Ayalagaya, Sabini John alimwabia mkuu wa mkoa kwamba, mafundi wa BAWASA mkoani hapo waliingia kwenye chanzo kinachotumika na wakazi wa vijiji hivyo na kuanza kufanya shughuli za kutaka kusambaza maji katika vijiji vingine bila kwanza elimu kwa wakazi wa vijiji husika.

Diwani John alieleza kuwa, mafundi hao bila taarifa walisababisha maji kuchafuka kwa kuchan’ganywa na saruji kitendo kilichowafanya vijana kuelekea sehemu ya chanzo hicho na kuwakuta mafundi hao ambao walichukuliwa hadi ofisi ya kijiji kwa kuchukuliwa maelezo ambayo hayakupokelewa hadi mkuu wa Wilaya ya Babati, Lazaro Twange kuingilia kati.

“Mafundi waliingia msituni kwenye chanzo bila kusaini kwenye ofisi ya kijiji, vijana waliopandisha kwenye chanzo na kuwakuta walikuwa wastaarabu sana, kwani hawakuwafanyia fujo yoyote zaidi ya kuwafikisha ofisini salama na hatimae kuwaruhusu waende hadi mwafaka upatikane,”amesema.

Aidha, mkuu wa mkoa alipokutana na wananchi wa vijiji hivyo jambo la kwanza aliwaruhusu watoe kero zao kwanza ndipo naye aweze kutoa majibu ya hoja zao bila kuathiri upande wowote na kuweza kupata mwafaka wa yaliyotokea na kusababisha taharuki kwa wakazi hao.

Kwa nyakati tofauti wanavijiji hao waliieleza DIRAMAKINI Blog kuwa, uamuzi wa watumishi hao kuingia katika mji wao bila kutoa taarifa ili kupewa ushirikiano ni dharau, hivyo wasingekubali kujishusha nao wasingekubali kutoa msamaha, kwani wanategemea maji hayo kwa matumizi mbalimbali ya kila siku.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news