Na Teresia Mhagama, WN-Kigoma
Waziri wa Nishati, January Makamba ameanza kutekeleza agizo lililotolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Philip Mpango tarehe 22 Septemba 2021 la kutatua changamoto ya kukatika umeme mara kwa mara mkoani Kigoma.
Katika ziara yake ya kikazi mkoani Kigoma aliyoifanya tarehe 06 Oktoba 2021, Waziri Makamba alibainisha kuwa, kuna mipango ya muda mfupi, kati na mrefu ambayo inalenga kuhakikisha kuwa Mkoa wa Kigoma unakuwa na umeme wa uhakika na hivyo kuondoa kero hiyo ya umeme kukatika mara kwa mara.
Waziri wa Nishati, January Makamba akiwa katika chumba cha kuongozea mitambo ya umeme katika Kituo cha kuzalisha umeme kilichopo Kigoma mjini tarehe 06 Oktoba, 2021. Kushoto kwa Waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Ester Mahawe.
Alibainisha kuwa, katika mipango ya muda mfupi, Kituo cha umeme cha Kigoma chenye uwezo wa megawati 6.25 kitaongezewa mashine mbili zitakazozalisha jumla ya megawati 2.5 kwenye kituo husika ambapo mashine ya kwanza yenye uwezo wa megawati 1.25 itakamilika kufungwa tarehe 15 Novemba 2021.
Aliongeza kuwa, mashine ya pili yenye uwezo wa megawati 1.25 itafungwa na kukamilika tarehe 25 Novemba 2021.
Aidha, alieleza kuwa miradi ya muda wa kati na mrefu itaunganisha Kigoma na umeme wa gridi na kupelekea Mkoa huo kuwa na umeme mwingi na wa bei nafuu kwani kwa sasa Kigoma inatumia umeme unaotokana na mafuta na hivyo inatumia shilingi Bilioni 3 kwa mwezi kuzalisha nishati hiyo huku mapato yakiwa ni shilingi bilioni 1.5.
Waziri wa Nishati, January Makamba (Wa Tatu kutoka kulia) akitazama moja ya mitambo ya kuzalisha umeme katika Kituo cha kuzalisha umeme kilichopo wilayani Kasulu mkoa wa Kigoma tarehe 06 Oktoba, 2021. Kushoto kwa Waziri ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji (Uzalishaji) kutoka TANESCO, Mhandisi Pakaya Mtamakaya.
Miradi hiyo ya muda wa kati na mrefu itakayounganisha Kigoma na gridi ya Taifa ni ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme itakayotoka Nyakanazi-Kakonko hadi Kibondo itakayokamilika Machi 2022
Mradi mwingine ni ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kV 132 kutoka Tabora hadi Kigoma ambayo inatarajiwa kukamilika Oktoba 2022.
Aidha, mradi mwingine ni ujenzi wa njia kubwa ya umeme ya msongo wa kV 400 kutoka Nyakanazi hadi Kigoma ambapo utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kukamilika mwaka 2023.
Waziri wa Nishati, January Makamba (Wa Tatu kutoka kulia) akiwa katika kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia Jua wilayani Kigoma Mkoa wa Kigoma kinachomilikiwa na kampuni ya Nextgen Solawazi. Kulia kwa Waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Ester Mahawe. Wengine katika picha ni Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Maharage Chande (wa kwanza Kushoto), na Wa Pili kutoka kushoto ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji (Uzalishaji) kutoka TANESCO, Mhandisi Pakaya Mtamakaya.
Vilevile mradi mwingine wa umeme unaotarajiwa kuboresha hali ya umeme mkoani Kigoma ni mradi wa kufua umeme wa maji wa Malagarasi utakaozalisha megawati 49.5 na Serikali imeshapata fedha kutoka Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) na mwakani atatafutwa mkandarasi kwa ajili ya ujenzi.
Akiwa mkoani Kigoma, Waziri Makamba alikagua mitambo ya kuzalisha umeme iliyopo wilayani Kigoma pamoja na wilayani Kasulu ambapo akiwa wilayani Kasulu alikuta changamoto ya mitaa mingi kukosa umeme ambapo ili kutatua changamoto hiyo alieleza kwamba utafanyika utaratibu ndani ya Wizara ili kuiwezesha TANESCO kupeleka umeme kwenye mitaa hiyo.
Waziri wa Nishati, January Makamba akizungumza na Wataalam kutoka TANESCO wanaofanya kazi katika Kituo cha kuzalisha umeme kilichopo wilayani Kasulu mkoani Kigoma wakati alipofika mkoani humo kutatua changamoto ya upatikanaji umeme wa uhakika.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Nishati alitembelea kituo cha umeme wa Jua cha Nextgen Solawazi ambacho kwa sasa kinazalisha umeme wa kiasi cha megawati 1.8 na kupeleka kwenye kituo cha kuzalisha umeme cha TANESCO ambapo kampuni hiyo ya Nextgen inatarajia kuongeza uzalishaji na kufikia megawati 4.3 ifikapo tarehe 8 Oktoba 2021.
Waziri wa Nishati, January Makamba (Wa Pili kushoto) akitazama baadhi ya mitambo ya umeme katika Kituo cha kuzalisha umeme kilichopo wilayani Kasulu mkoa wa Kigoma tarehe 06 Oktoba, 2021. Kushoto kwa Waziri ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji (Uzalishaji) kutoka TANESCO, Mhandisi Pakaya Mtamakaya na kulia kwa Waziri ni Mkuu wa Kituo cha umeme cha Kasulu, Masanja Nkuba.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TANESCO, Maharage Chande, alisema kuwa, Mkoa wa Kigoma utaanza kupata umeme wa gridi ya Taifa ifikapo Machi 2022.
Katika ziara hiyo Waziri wa Nishati aliambatana na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Kigoma wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Ester Mahawe ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.