Na Robert Kalokola,Geita
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa, ni upotoshaji kudai kuwa viongozi wa Mbio za Mwenge wanakufa baada ya kumaliza kukimbiza Mwenge kwani viongozi wengi waliowahi kukimbiza bado wako hai hadi sasa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akihutubia katika Maonesho ya Vijana wilayani Chato. (Picha na Robert Kalokola).
Viongozi wastaafu wa Mbio za Mwenge wakiwa kwenye banda la Jumuiya ya Wakimbiza Mwenge Wastaafu (TAUTA) kwenye Maonesho ya Wiki ya Vijana wilayani Chato. ( Picha na Robert Kalokola)
Amesema kuwa, baadhi ya watu wanaoeneza taarifa hizo hawana nia njema na taifa kwasababu viongozi hao wa kukimbiza Mwenge wanafanya kazi kubwa ya kuhamasisha shughuli mbalimbali za jamii kama mapambano dhidi ya malaria,rushwa na utapiamlo.
Waziri Mhagama amesema hayo wilayani Chato katika Maonesho ya Wiki ya Vijana Kitaifa alipotembelea Banda la Jumuiya ya Wakimbiza Mwenge wastaafu katika viwanja vya Mazaina.
Amefafanua kuwa, baadhi ya viongozi wa Mbio za Mwenge bado wako hai na wanaendelea kuishi kama binadamu wengine na taarifa kwamba wanakufa ni uongo wenye nia mbaya.
Jenista Mhagama ameongeza kuwa amekutana na Viongozi wa miaka ya nyuma ambao waliwahi kukimbiza mwenge wa Uhuru na bado wako hai na wameanzisha Jumuiya yao ili waendelee kurithisha uzalendo waliupata katika shughuli hiyo.
Ameongeza kuwa, Mbio za Mwenge wa Uhuru zinatumika kuhamasisha amani,mshikamano na uzalendo pamoja kukagua miradi ya maendeleo .
Mwenge wa Uhuru Umepokelewa mkoani Geita Oktoba 9, 2021 kutoka Mkoa wa Kagera na unatarajiwa kuzimwa Oktoba 14, mwaka huu wilayani Chato na Rais Samia Suluhu Hassan.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Jumuiya ya Wakimbiza Mwenge Wastaafu, Mwashibanda Shibanda amesema kuwa, jumuiya hiyo imeanzishwa ili kuendelea kutoa elimu ya uzalendo,amani na utulivu kwa vizazi vilivyopo na vijavyo kwa maslahi ya taifa.
Amefafanua kuwa, ni upotoshaji kueleza kuwa viongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru wanakufa baada ya mbio hizo kuisha.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (kulia) akikagua mabanda mbalimbali katika maonyesho ya vijana Chato, kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule. (Picha na Robert Kalokola).
Amesema kuwa,jambo ambalo linaweza kusababisha kifo ni ajali ikitokea kama inavyotokea sehemu nyingine ambazo siyo mbio za Mwenge.
Jumuiya hiyo ya Wakimbiza Mwenge wastaafu katika banda hilo kwenye maonyesho ya Wiki ya Vijana imekusanya viongozi waliowahi kukimbiza mwenge kuanzia mwaka 1988.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Chum Ababala Abdalla amesema kuwa malengo ya mwenge mwaka 1988 ilikuwa kuhamasisha mapambano ya janga la ugonjwa wa Ukimwi pamoja na uharibifu wa mazingira kwa kukata miti.
Amefafanua kuwa, mwaka huo kulikuwa na wimbi kubwa la ukataji miti nchi katika maeneo mbalimbali iliyotishia nchi kuingia kwenye jangwa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akiwa amepanda gari ambalo limetengenezwa na vijana wa Chato( Picha na Robert Kalokola)
Amesema kuwa baada ya mbio za Mwenge kukimbia nchi nzima na kuhamasisha upandaji miti uoto umebadilika kwasababu miti ilipandwa ya kutosha.
Maonesho ya Wiki ya Vijana yameanza Oktoba 8, mwaka huu na yatafunguliwa rasmi na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Oktoba 12, mwaka huu na yatahitimishwa siku ya kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru ambapo Rais Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi katika kuzima Mwenge wa Uhuru 2021.