NA MWANDISHI MAALUM
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi maafisa mapato watatu wa Halmashauri ya wilaya ya Kilwa na kuiagiza Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) pamoja na Jeshi la Polisi wawachunguze na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
“Hatuwezi kuwa na watumishi wa umma walioaminiwa na Mheshimiwa Rais amewaleta hapa Kilwa kuwatumikia wananchi mkusanye mapato yakajenge zahanati, shule na visima vya ninyi mnakula tu, haiwezekani, sasa nawasimamisha kazi. Polisi na TAKURURU nendeni makawachunguze na kuwafikisha mahakamani”
Waziri Mkuu amewasimamisha kazi watumishi hao leo Oktoba 6,2021 wakati akizungumza na madiwani, watumishi na wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa akiwa kwenye ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo katika mkoa wa Lindi. Watumishi waliosimamishwa kazi ni Bahaye Shilungushella, Ally Kijonjo na Mohamed Samodu.
Amesema katika mkutano mkuu wa ALAT Taifa, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alikemea na kusisitiza hatua kali zichukuliwe kwa watumishi wote watakaobanika kujihusisha na matumizi mabaya ya fedha za Umma.
“Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa ina jumla ya mashine 97 za kukusanyia mapato lakini kati yake zinazofanya kazi ni mashine 55 tu, sasa nielezeni maeneo mengine ambayo mashine zake 42 hazifanyi kazi fedha zinaenda wapi”
Pia, Waziri Mkuu amewaagiza Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmshauri ya Kilwa wahakikishe fedha zote zinazokusanywa katika halmshauri hiyo zinakwenda kutekeleza miradi ya maendeleo ili kuwanufaisha wananchi. “Simamieni vizuri miradi inayotekelezwa na muhakikishe viwango vya ubora vinaendana na thamani ya fedha iliyotolewa”
Aliongeza kuwa Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia imejidhatiti kuwahudumia Watanzania kwa kufikisha huduma muhimu za kijamii mahali walipo, hivyo watumishi wa umma wahakikishe wanajenga misingi ya kwenda kuwahudumia wananchi “Rais Samia anataka kuona wananchi wanahudumiwa ipasavyo.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema Pia amewataka watumishi hao wahakikishe wanafanya kazi ya kutoa huduma kwa wananchi kwa kufuata taratibu zilizowekwa pamoja na kusimamia vizuri fedha za miradi ya maendeleo zinazopelekwa katika maeneo yao.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kuwa katika kipindi cha kuanzia mwezi Machi, 2021 hadi Juni, Rais Samia ametoa shilingi bilioni 5.8 kwa ajili ya sekta ya elimu mkoani Lindi. “Wilaya hii ya Kilwa imepokea shilingi milioni 700 kwa ajili ya sekta ya elimu.