NA MWANDISHI MAALUM
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imetenga shilingi bilioni 170 kwa ajili ya ujenzi wa Mkongo wa Taifa katika mwaka wa fedha 2021/2022 huku pia akisisitiza umuhimu wa mifumo ya usalama kupitia TEHAMA katika miji mbalimbali hapa nchini.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (katikati – walioketi) akiwa kwenye picha ya pamoja wadau mbalimbali wa Mkutano wa Tano wa Mwaka wa TEHAMA Tanzania uliofanyika katika katika ukumbi wa mikutano wa AICC, jijini Arusha wakiwemo viongozi waandamizi wa serikali na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Huawei Tanzania Bw. Damon Zhang (wa pili kulia – waliosimama).
Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo Oktoba 22, 2021 wakati alipofungua Mkutano wa Tano wa Mwaka wa TEHAMA Tanzania uliofanyika katika katika ukumbi wa mikutano wa AICC, jijini Arusha.
Kuhusu Mkongo wa Taifa, Waziri Mkuu Majaliwa amesema fedha hizo zitawezesha kujenga kilomita 4,244 za Mkongo huo ili kufikisha jumla ya kilomita 12,563.
“Lengo letu ni kuwawezesha watoa huduma za mawasiliano kutumia miundombinu hii kuboresha huduma za mawasiliano nchini na kurahisisha ufikishwaji wa intaneti kwenye ofisi mbalimbali za sekta ya umma na binafsi”
Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuiagiza Wizara ya Habari, Sayansi na Teknolojia ya Habari isimamie kwa karibu mradi wa upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili wananchi wengi zaidi washiriki katika ujenzi wa uchumi wa kidijitali.
“Hivi sasa Serikali imejenga kilomita 8,319 za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano hadi mwezi Septemba 2021. Malengo yetu kama Serikali ni kujenga hadi kilomita 15,000 ifikapo mwaka 2024/2025. Hili linahitaji uwekezaji mkubwa na Serikali imejipanga kuwekeza vilivyo lakini pia tunakaribisha wabia na wawekezaji katika eneo hili pamoja na maeneo mengine ya TEHAMA.” alisema
Kuhusu umuhimu wa uwepo wa mifumo ya usalama kupitia TEHAMA katika miji mbalimbali hapa nchini, Waziri Mkuu alisema zitasaidia kuongeza usalama kwa kuwa utawezesha kuwa na rekodi za matukio mbalimbali yakiwemo yakihalifu katika maeneo hayo.
“Nilipata nafasi ya kufanya ziara China na nikatembelea ilipo kampuni ya Huawei, hapo nilijionea teknolojia kubwa na za kisasa ambazo tunaweza kuzitumia hapa nchini pia’’ Alisema Waziri Mkuu Majaliwa
Baada ya kufungua mkutano huo Mheshimiwa Majaliwa pia amezindua mwongozo wa usajili wa wataalamu wa TEHAMA na kutoa vyeti kwa baadhi ya wataalamu wa TEHAMA ambao wamesajiliwa
Kwa upande wake Waziri wa Habari, Sayansi na Teknolojia ya Habari Dkt. Ashatu Kijaji amesema wizara yao imejipanga kujenga kituo mahiri cha kukuza utaalamu na tafiti nchini ambacho kitajengwa jijini Dodoma kwa kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali “Digital Tanzania”.
Miongoni mwa waliotunukiwa tuzo ni pamoja na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kulibeba suala la TEHAMA kwa nguvu zake zote na kuliweka kwenye vipaumbele vya Serikali ya awamu ya sita ambayo anaiongoza.
Awali, katika mahojiano yake na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi huo Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Huawei Tanzania Bw. Damon Zhang alisema kampuni hiyo ipo tayari na imejitolea kufanya kazi na serikali katika kuleta maono ya pamoja ya kukuza uchumi wa kidijiti, sambamba na kudhibiti changamoto zilizoletwa na ustawi wa Tehama.
“Tunajitolea kuendelea kukuza ujumuishaji wa kidijiti kwa kila mtu, kila nyumba, na k ila shirika kwa ajili ya kuandaa Tanzania iliyounganishwa.’’ Alisema Bw Zhang huku akiongeza kuwa ipo haja ya kuwekeza zaidi huduma ya TEHAMA katika maeneo ya vijijini ili kuinuia sekta ya kilimo ambayo ustawi wake kwa kiasi kikubwa unahitaji huduma .