Waziri Ndumbaro:Kampeni ya Royal Tour haipoi, tunakuja na mkutano wa masoko na utalii wa Kimataifa

NA LUSUNGU HELELA-WMU

Kabla ya Kipindi maalum cha kutangaza utalii maarufu cha ‘Royal Tour’ kilichoanzishwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan hakijapoa kwa mara nyingine tena, Wizara ya Maliasili na Utalii imesema inatarajia kufanya mkutano mkubwa wa Kimataifa wa Utalii na Masoko (Tourism Marketing) katika Jiji la Arusha, wiki ya pili ya mwezi Novemba mwaka huu.
Waziri wa Maliaslili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro akizungumza kuhusiana na kufanyika kwa mkutano wa kimataifa wa utalii na masoko wakati akifanya mahojiano maalum ya jinsi Wizara ya Maliasili na Utalii ilivyojipanga kutangaza vivutio vya utalii ilivyonavyo kimataifa kwa lengo la kuongeza idadi ya watalii nchini kutoka watalii milioni 1.5 hadi kufikia watalii milioni 5 kama ilani ya CCM inavyoelekeza ifikapo mwaka 2025

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro ametoa kauli hiyo leo Jijini Dar es Salaam wakati akifanya mahojiano maalum ya jinsi Wizara hiyo ilivyojipanga kutangaza vivutio vya utalii ilivyonavyo kimataifa kwa lengo la kuongeza idadi ya watalii nchini kutoka watalii milioni 1.5 hadi kufikia watalii milioni 5 kama ilani ya CCM inavyoelekeza ifikapo mwaka 2025.

Waziri Ndumbaro amesema lengo la mkutano huo utakaofanyika kwa muda siku mbili utajadili namna ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini kwa kuwakutanisha wadau wa utalii wa ndani na nje ya nchi wakiwemo wamiliki wa makampuni ya Kimataifa ya kutangaza utalii duniani pamoja na Wataalam kutoka Shirika la Umoja wa Kimataifa linaloshughulikia masuala ya utalii Duniani ( UNWTO).

Akizungumzia Washiriki hao, Dkt.Ndumbaro amesema mkutano huo wa kimataifa utatoa fursa kwa Washiriki duniani kote hata kwa wale watakaoshindwa kufika nchini wataweza kushiriki kwa njia ya mtandao pia.

Akizungumzia sababu iliyopelekea Wizara hiyo kuamua kufanya mkutano huo, Dkt.Ndumbaro amesema kama nchi imejaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii na vya kipekee ambavyo havipatikani mahali popote duniani isipokuwa Tanzania lakini vivutio hivyo vimekuwa havijulikani Kimataifa.

”Nilipofika Wizarani baada ya kufanya kazi kwa muda wa mwezi mmoja tu nikawambia wenzangu kwamba kama ningekuwa natoa ‘marks’ kwenye maeneo mawili kwenye uhifadhi na utalii, kwenye uhifadhi ningetoa marks mia kwa mia lakini kwenye utalii ningetoa moja ya mia kwani kwa vivutio vya utalii tulivyonavyo Tanzania tumeshindwa kuvitangaza, tungevitangaza vizuri mapato yetu yangekuwa sio ya hapa,”amesisitiza Dkt.Ndumbaro.

Dkt.Ndumbaro amesema nchi ya Tanzania katika suala la vivutio vya utalii ipo vizuri ila kwenye suala la ”marketing” ya vivutio vya utalii haipo vizuri.

“Tunaona kwenye suala la kujitangaza ndio kuna ugonjwa ndio maana Mimi na Wenzangu tunajitahidi kupigania kuleta mikutano mikubwa ifanyike nchini pamoja na kuanzisha mazao mengine ya utalii kama njia kutangaza vivutio vya utalii tulivyonavyo,” amesisitiza Dkt.Ndumbaro.

Dkt.Ndumbaro amesema uamuzi wa kufanya mkutano huo wa masoko na utalii ni moja ya mikakati maalum ambayo kama Wizara ni kuhakikisha jitihada alizozianzisha Rais Samia Suluhu Hassani za kuitangaza utaliii nchini kupitia kipindi chake maarufu cha “Royal Tour” hazipoi na kusisitiza kuwa kampeni hiyo inazidi kuwa ya moto kila kukicha.

Kufuatia hali hiyo, Dkt.Ndumbaro ametoa wito kwa sekta binafsi kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha mkutano huo unafanikiwa kufanyika ili sekta ya utalii iweze kuinuka tena kufuatia wimbi la UVIKO-19.

Amesema mkutano huo utakuja na mbinu mbadala kwa kuhakikisha sekta ya utalii nchini inapaa kwa kuyafanyia kazi mawazo yatakayotolewa katika mkutano huo haraka kadiri iwezekanavyo ili kuongeza idadi ya watalii wa ndani na nje ya nchi.

Katika hatua nyingine, Dkt.Ndumbaro amesema kufanyika kwa mkutano huo kutasaidia kujua udhaifu upo wapi katika kutangaza vivutio vya utalii nchini kwa kuweza kuondokana na taswira mbaya ambayo muda mwingine imekuwa ikifanywa na baadhi ya watu kwa maslahi yao binafsi

Amesema, kuna baadhi ya watu wamekuwa wakiharibu taswira ya nchi kwa maslshi yao binafsi na huku wengine kwa sababu za kisiasa bila kujua hali hiyo imekuwa ikiiathiri sekta ya utalii moja kwa moja.

”Kuna baadhi ya Watanzania ambao ni wapuuzi wamekuwa wakijisikia fahari kuisema nchi yake vibaya na kuisifia nchi nyingine vizuri,” alisitiza Dkt.Ndumbaro.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news