Waziri Prof.Mkenda: Tushiriki kikamilifu Sensa ya majaribio na ile ya Kitaifa mwakani

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

WAZIRI wa Kilimo, Prof.Adolf Mkenda ametoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Ruvuma na Tanzania kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika zoezi la sensa ya majaribio katika maeneo itakapofanyika na hatimaye sensa ya kitaifa mwakani.

Rai hiyo alimeitoa leo Oktoba 13, 2021 wakati akitoa hotuba kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani ambayo yamefanyika katika Uwanja wa Majimaji mkoani Ruvuma.

"Zoezi hili litasaidia kupata takwimu sahihi zitakazosaidia Serikali katika upangaji wa mipango yake ya maendeleo. Uwepo wa takwimu sahihi kunasaidia sana katika upangaji wa mipango na hivyo kuwa na mipango inayotekelezeka kwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,"amebainisha Waziri Prof. Mkenda.

Mbali na hayo, Waziri Profesa Mkenda amesema kuwa, jitihada za kuhakikisha Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi zinazojitosheleza kwa chakula duniani ilianza tangu kupata Uhuru mwaka 1961 ambapo muasisi wa Taifa letu Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitangaza taifa hili kuwa Taifa la wakulima na wafanyakazi.

"Mara zote Mwalimu alisisitiza watanzania kujikita katika kilimo bora kwa ajili ya maendeleo yao binafsi na Taifa. Hili limedhihirika katika maazimio au kauli mbiu zikiwemo “Siasa ni kilimo, kilimo cha kufa na kupona, azimio la Arusha, Kilimo cha kisasa na nyingine,"mesema.

Amesema, tangu wakati huo, Serikali imekuwa ikichukua juhudi mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha wakulima wanafanya kilimo chenye tija na hivyo kuwanufaisha wakulima mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Miongoni mwa jitahada hizo ni pamoja na kuhakikisha wakulima wanapata na kutumia mbolea stahiki katika uzalishaji wa mazao.

Aidha, amesema hivi karibuni bei ya mbolea katika soko la Dunia ilipanda na serikali ilichukua hatua za haraka kuruhusu wafanyabiashara kuagiza mbolea na kuuza kwa bei shindani ili kumuwezesha mkulima kupata mbolea kwa bei atakayomudu.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani mwaka 2021 inasema “Tumia mbolea Bora kwa Tija na Kilimo Endelevu”.

Waziri Prof.Mkenda amesema, kaulimbiu hiyo inatoa ujumbe mahsusi kwa wakulima ambao ndio tegemeo kwa uzalishaji wa chakula nchini na nchi jirani.

"Pamoja na ukweli kwamba wakulima hawa ndio wazalishaji wakuu, bado kuna changamoto zinazosababisha wakulima kuwa na tija ndogo ya uzalishaji.

"Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na matumizi madogo na yasiyo sahihi ya mbolea yanayotokana na utumiaji wa mbolea pasipo kutambua afya ya udongo. Sababu zingine ni matumizi ya mbegu zenye viwango vidogo vya ubora, magonjwa ya mimea na mabadiliko ya tabia nchi yanayosababisha ukame, mafuriko na au milipuko ya visumbufu vya mimea.

"Aidha, matumizi ya zana duni za kilimo unaofanya gharama za uzalishaji kuwa kubwa, miundombinu hafifu ya usafirishaji wa mazao kutoka mashambani hadi kwa watumiaji, ukosefu wa mifumo ya taarifa za masoko unaofanya wakulima walanguliwe na ukosefu wa viwanda vya kuchakata mazao ili kuyaongezea thamani pia ni miongoni mwa sababu zinazo fanya kilimo kutokuwa na tija,"amesema Waziri.

Alibainisha kuwa, katika jitihada za kumkwamua mkulima na changamoto zilizoorodheshwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuruhusu wafanyabiashara kuagiza mbolea kwa bei ya soko na kuuza kwa bei shindani ili kuruhusu mkulima kupata mbolea kwa bei atakayoimudu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news