NA MOHAMED HAMAD
Ziara ya mawaziri nane wakiongozwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi mkoani Manyara imeleta matumaini makubwa kwa wananchi wa vijiji vya Kimotoroko wilayani Simanjiro na Makame wilayani Kiteto mkoani Manyara.
Awali wananchi hao wanaopakana na hifadhi za Tarangire na Pori la Akiba la Mkungunero walidai kuwa na mgogoro wa muda mrefu uliosababisha kupata madhara, kuporwa mifugo, kuteswa na askari wa hifadhi hizo.
Mwananchi, Leah Saitoti amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuagiza timu hiyo ya Mawaziri hao nane ambao alidai wamefanya kazi nzuri ambayo imewarudishia ardhi yao kwa sasa wanafuga, wanalima tofauti na wakati wa mgogoro huo ambapo wakienda kukata kuni ama kuchota maji walikamatwa na kuteswa.
"Askari wa Pori la Akiba Mkungunero, lililopo wilayani Kondoa wamekuwa wakitukamata, kutupiga na kutesa na hata kutufungulia kesi ambazo zinatusumbua," amesema Leah.
Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Kimotoroko, Patern Kivuyo amesema, tamko la mawaziri nane wakiongozwa na Mhe. William Lukuvi, kutaka wamiliki wa hifadhi za Tarangire na Pori la Akiba la Mkungunero kutobughudhi wananchi limewapa faraja kubwa na sasa hawakamatwi, wala kuteswa tena.
"Mawaziri nane walipofika tarehe Saba walisema, tatizo limeisha, wakatoa ekari 4,392.5 za hifadhi ya Tarangire na kuwakabidhi wananchi ambao awali waliishi kwa tabu baada ya kuporwa ardhi hiyo," amesema Kivuyo.
Naye Edward Ndoki wa Kijiji cha Lobosireti amesema, mifugo yake 131 ilikamatwa kwenye eneo ambalo linadaiwa ni hifadhi na kutozwa faini ya Shilingi Milioni 7.4 na baada kuachiwa ng'ombe saba zilikufa akisema huo ulikuwa ukatili wa hali ya juu.
Amesema awali eneo hilo walilitumia kama nyanda za malisho, hata wanyama kwao hawakuwa ni tatizo walipishana nayo kama kawaida hivyo kitendo cha kutakiwa kuondoka humo huku wakiwa na miaka mingi kinawagharimu kwa kuwa hawana pakwenda.
Akizungumzia eneo hilo Julius Venance Peter Msofe mpima Kutoka Wizara ya Ardhi makao makuu ya Dodoma alisema, walifika baada ya Mawaziri hao nane kutoa tamko kutaka eneo hilo lipimwe upya na kutambuliwa makazi ya wananchi sambamba na kushauri namna bora ya wao kuishi
Alitaja changamoto iliyopo katika maeneo hayo kuwa ni mgogoro wa mpaka kati ya Mkoa wa Manyara na Dodoma akisema wao wanachofanya ni kuangalia namna bora ya kufanya ili wananchi waishi salama tofauti na maisha yao ya awali.
Pascal Mrina mjumbe wa timu iliyoundwa na Mwenyekiti wa Mawaziri hao wakiongozwa na Mhe. William Lukuvi alitaka Kijiji cha Ilkiushbar wilayani Kiteto kuwa moja kati ya maeneo yenye mgogoro na Pori la Akiba la Mkungunero hivyo wamefika kufanya tathmini kuona maisha ya wananchi hao makazi yao yalivyo kwenye mapito ya wanyama na mahitaji yao.
"Hatua hii ni nzuri ndio itakayoenda kumaliza mgogoro hii ambayo imekuwa madhara mara zote kwani mara baada ya kwisha kila upande utakuwa na eneo lake kisheria," amesema.