NA IMMA MSUMBA
Wanawake 307 waishio mkoani Arusha wamefanyiwa uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road katika Wiki ya Maadhimisho ya kudhibiti na kupambana na magonjwa yasiyoambukiza iliyofanyika kitaifa katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Meneja wa Kitengo cha Uchunguzi wa Saratani kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road,Dokta Maguha Stephano amesema Novemba 12, 2021 kuwa wamekuwa na zoezi la kufanya uchunguzi wa awali wa saratani ya mlango wa kizazi ,saratani ya matiti pamoja na kupima tezi dume kwa wanaume.
Dokta Maguha amesema kuwa, wanawake 7 kati ya 307 waliofanya uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi wamekutwa wana mabadiliko ya awali na wamepatiwa matibabu huku wawili wamekutwa na viashiria vya saratani ya mlango wa kizazi hivyo wamepewa rufaa ya kwenda KCMC.
“Kwenye uchunguzi wa saratani ya matiti wanawake 307 wamefanyiwa uchunguzi ambapo wanawake 5 wameonekana wana vivimbe kwenye matiti,pia wanawake 3 wameonekana wana viashiria vya saratani ya matiti,”amesema Dkt. Maguha.
Hata hivyo amesema kuwa jumla ya wanaume 277 wamejitokeza kufanyiwa uchunguzi wa tezi dume kwa njia ya kupima damu ambapo wanaume 5 wamekutwa na viashiria vya kuwa na saratani ya tezi dume.
Dokta Maguha anawashauri wananchi kujenga tabia ya kufanya uchunguzi wa afya zao mara kwa mara ili waweze kujua afya zao na kuchukua hatua stahiki.
Uchunguzi wa Magojwa ya Saratani ya Mlango wa kizazi na matiti pamoja na uchunguzi wa tezi dume unaandelea kufanyika hadi leo Novemba 13 ,2021 katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.