NA ABUBAKARI KAFUMBA-UAE
MSANII Abby Chams kutoka Tanzania ametembelea banda la Tanzania kwenye maonesho ya Expo 2020 Dubai ambapo alipokelewa na Kamishna Jenerali wa Banda la Tanzania kwenye maonesho ya Expo 2020 Dubai Mhe. Balozi Mohammed Abdallah Mtonga na Mkurugenzi wa Banda la Tanzania Bi. Getrude Ng’weshemi kutoka TanTrade pamoja na wawakilishi wa Sekta mbalimbali zinazoshiriki kwenye maonesho haya.
Baada ya kupokelewa Abby Chams alitembezwa kwenye banda la Tanzania akiongozwa na Mkurugenzi wa Banda kujionea mambo mbalimbali yaliyopo kwenye banda na kujifunza namna ambavyo Tanzania imetumia fursa ya ushiriki kwenye maonesho haya ya Expo 2020 Dubai kutabgaza upekee wake, vivutio mbalimbali na fursa kubwa zilizopo nchini.
Ndani ya banda la Tanzania muonekano wa maudhui wake umesheheni maudhui mbalimbali yanayoitangaza Tanzania kupitia sekta mbalimbali zilizopewa kipaumbele ambazo ni Utalii, Madini, Kilimo, Miundombinu na Miradi mikubwa ya kimkakati.
Zoezi hili la kutembelea banda la Tanzania lilienda sambamba na tukio maalum lililoandaliwa kwa msanii Abby Chams ambapo Kamishna Jenerali wa Banda la Tanzania Mhe. Balozi Mohammed Abdallah Mtonga alitumia fursa hiyo kuongoza tukio hilo kwa kumkaribisha Abby Chams kwenye eneo ambalo banda la Tanzania inaonyesha madini ya ‘Tanzanite’.
Mhe. Balozi Mtonga alisema kuwa,”fursa aliyoipata Abby Chams kutembelea katika banda letu leo akiwa kama kijana anayeiwakilisha na ambaye ameiwakilisha vema Tanzania hapa kwenye maonesho haya ya Expo 2020 napenda kutumia nafasi hii ya uwepo wake kama alama ya kufungua rasmi eneo la ‘Tanzanite’ kwenye banda letu ambapo tutakuwa tunauonesha Ulimwengu upekee wake ili waweze kuja kujifunza na kujionea dhahiri sio tu wabaki kuisikia. Kwa upekee wake madini haya yanapatikana Tanzania peke yake kote ulimwenguni. Kupitia zoezi hili pia ninafungua rasmi duka la kuuza ‘Tanzanite’ ndani ya banda la Tanzania ambalo litauza vito mbalimbali vya thamani katika maonesho ya Expo 2020 Dubai kupitia kampuni ya The Tanzanite Experience kutoka Tanzania inayojishuhulisha na uuzaji wa vito vya thamani vya ‘Tanzanite’ na kuielimisha jamii kuhusu chanzo cha madini hayo ikiwa ni Tanzania peke ulimwnguni kote”.
Baada ya tukio hilo la kufungua eneo la ‘Tanzanite’ kwa kukata upete Balozi Mtonga alimkabidhi Abby Chams zawadi ya ‘Uru Tanzanite Bracelet’ kutoka The Tanzanite Experience kama ishara ya kuvutia uhamasishaji kwa wote kwenye maonesho haya kuja kwa wingi kwenye banda la Tanzania kujionea upekee wa ‘Tanzanite’.
Aidha, Mkurugenzi wa Banda la Tanzania Bi. Getrude Ng’weshemi amesema kuwa,” Abby Chams akiwa kijana mzalendo wa kitanzania tunafurahi kuweza kujumuika nae hapa kwenye banda letu. Tuko nae bega kwa bega katika kuipeperusha bendera ya Tanzania ulimwenguni na huu ni mwanzo tu wa kushirikiana nae kuufikia ulimwengu na kuleta hamasa ya uzalendo wa vijana wa kitanzania na watanzania wote walio ndani na nje ya nchi. Hekima, Umoja, Amani, ndio ngao zetu”.
Msanii Abby Chams nae alipata fursa ya kuzungumza kwa ufupi kumshukuru Kamishna Jenerali wa Banda la Tanzania Mhe. Balozi Abdallah Mtonga na Mkurugenzi wa banda Bi. Getrude Ng’weshemi kwa kupewa fursa hii kuwa sehemu ya tukio hilo muhimu. Alisema,” nafarijika sana kuona nchi yangu imesimama miongoni mwa nchi 192 ambazo zinashiriki katika maonesho haya ya Expo 2020 Dubai. Ni vema tukatumia fursa hii kama nchi kuufikia ulimwengu na kuujulisha jinsi Tanzania ilivyobarikiwa. Binafsi naipenda sana nchi yangu Tanzania na zoezi hili la leo limenivisha taji la uzalendo na hii ni motisha kwa Tanzania na Watanzania wote kutumia nafasi hii kama jukwaa la kujenga uhusiano endelevu kwa kujichanganya na mataifa mengine kwani hii kwetu kama taifa ni heshima kubwa itakayo acha alama Ulimwenguni na jina la nchi yetu Tanzania likibaki linatajwa na wengi”.
Baada za zoezi hilo kumalizika Abby Chams alionesha uzalendo mkubwa kwa kuimba wimbo wa Taifa akidhihirisha uzalendo wake na ushikiri katika tukio hilo na maonesho ya Expo 2020 Dubai akiiwakilisha Tanzania.
Matarajio ya wengi ni ya Tanzania kufika mbali kwa pamoja kama nchi. Tuendelee kuwa wazalendo kuiwasilusha nchi yetu kwenye maonesho haya kwa uhakika kwa watanzania wote walio ndani na nje ya Tanzania. Tutumie ushiriki wetu kwenye maonesho haya kuketa maendeleo yenye tija kwa taifa letu kwa ujumla.