Ajali ya ghorofa iliyoua 36, yaacha vilio na simanzi

NA GODFREY NNKO

Idadi ya miili iliyopatikana kutoka katika jengo la ghorofa lililoporomoka katika jiji lenye watu wengi zaidi nchini Nigeria la Lagos imeongezeka hadi kufikia 36.
Miongoni mwa wanawake ambao wamepoteza ndugu zao katika ajali hiyo ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa akiangua kilio. (Picha na Sunday Alamba/AP)

Hayo yamebainishwa na Ibrahim Farinloye kutoka Shirika la Taifa linalojishughulisha na Usimamizi wa Dharura la Nigeria katika mahojiano na AP.

Farinloye amesema, miili 15 zaidi imepatikana kutoka eneo la ajali ikiwa ni pamoja na miili miwili iliyoripotiwa mapema na AP.

Juhudi za uokoaji zilipoingia siku ya nne jana Alhamisi, matumaini yalianza kuwa finyu kwa familia nyingi na wakazi waliojipanga kwenye lango la jengo hilo na kuomba wajiunge na juhudi za uokoaji, wakipuuza maonyo ya askari waliokuwa na bunduki kwamba wanapaswa kukaa mbali kutoka eneo la tukio.

"Hawakuweza kuniruhusu kuangalia kama mwanangu yuko hai au amekufa," alisema Abel Godwin, ambaye alisafiri kilomita 722 kutoka mji mkuu wa taifa hilo, Abuja, kuangalia hospitalini ambapo waathiriwa wanatibiwa. Ni mtoto wa miaka 18 ambaye alikuwa ameajiriwa kwenye eneo hilo.

Hakuna manusura waliookolewa kutoka kwenye rundo la vifusi tangu Jumanne, huku tisa kati ya wale waliotolewa wakiwa hai mapema wakiwa katika hali ya matumaini.

Jengo hilo la kisasa lenye ghorofa 21 lililokuwa likijengwa liliporomoka Jumatatu wakati wafanyakazi wa ujenzi wakiwa kwenye eneo hilo, ambao baadhi yao walikuwa mafundi walioanza kazi siku hiyo.

Haijulikani ni watu wangapi ambao bado wamenaswa ndani ya vifusi, lakini mfanyakazi mmoja wa ujenzi katika eneo la tukio alikadiria kuwa watu 100 walikuwa wakifanya kazi hapo lilipoporomoka, ikimaanisha kuwa watu 55 bado wanaweza kuwa humo ndani ya vifusi.

Segun Akande wa Shirika la Msalaba Mwekundu la Nigeria ameiambia AP kwamba, ingawa juhudi za uokoaji zinaendelea,bado matumaini ni madogo kuwapata waliopo ndani wakiwa hai.
Waokoaji na wasamaria wema wakiendelea na juhudi za kutafuta miili ya watu katika maporomoko ya ujenzi huo mjini Lagos, Nigeria. ( Picha na Sunday Alamba/AP).

Jengo hilo lilipoporomoka, ilichukua takriban saa 3 kwa maafisa kuanza shughuli ya uokoaji. Hali hiyo iliwapa hasira wakazi na familia ambazo zililalamika zaidi kwamba utafutaji wa ndugu zao haupewi uzito vya kutosha.

Gavana wa Lagos ametoa siku 30 kwa jopo huru kubaini chanzo cha ajali hiyo na iwapo waendelezaji wa mradi huo walikuwa wamefuata sheria za ujenzi kikamilifu.

Jopo hilo la watu sita pia litachunguza ikiwa kulikuwa na mapungufu yoyote na wadhibiti wa serikali katika kusimamia mradi huo.

"Tunahisi wasiwasi mwingi wa wanafamilia. Watu wamekasirika kweli," Gavana Sanwo-Olu aliwaambia waliokuwepo kwenye eneo hilo siku ya Jumatano na kuongeza kuwa, "Ninaweza kuwahakikishia tunafanya kila kitu," alisema, akiahidi kwamba mashtaka ya uhalifu yatafunguliwa dhidi ya wale watakaoshtakiwa kuhusika katika maafa hayo.

Majengo yanaporomoka nchini Nigeria mara kwa mara, ikiwa ni pamoja na Lagos ambayo ilirekodi ajali nne za aina hiyo mwaka jana, na kusababisha majeruhi watano ikiwa ni pamoja na watoto watatu.

Mamlaka iliendelea kukabiliwa na shinikizo kubwa juu ya tukio la hivi karibuni huku kukiwa na tuhuma kwamba walikosa kutii maonyo ya hapo awali na kupitisha mapendekezo yenye mashaka.

"Nadhani kuna maabara moja tu ya upimaji huko Lagos. Mapendekezo yalitolewa zaidi ya miaka 10 iliyopita, hebu tuwe na maeneo mengine ya upimaji wa maabara yaliyoidhinishwa,” alisema David Majekodunmi, Mwenyekiti Taasisi ya Wasanifu Majengo ya Nigeria huko Lagos.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news