NA MWANDISHI MAALUM
MBUNGE wa Jimbo la Dodoma Mjini mkoani Dodoma, Mheshimiwa Anthony Mavunde amezindua rasmi Umoja wa Familia ya Wanamichezo wa Zamani Dodoma (UFAWAZA) na kupewa heshima ya kuwa mwanachama wa kwanza wa heshima.Uzinduzi huo umefanyika katika Hoteli ya Royal Village Dodoma na kuhudhuriwa na wanamichezo mbalimbali wa zamani ambao Mbunge Mavunde amejitolea kuwalipia bima ya jamii kwa miaka miwili itakayogharimu sh.milioni 4,000,000 kupitia Benki ya Biashara Tanzania (TCB).
“Nawashukuru wazee wangu kwa kunipa heshima hii kubwa ya kuwa mmoja wa wanafamilia na kuwa mwanachama wa kwanza wa heshima wa UFAWAZA.
"Nawapongeza kwa kuja na wazo hili la kuunda umoja huu wa kuwakutanisha wachezaji wa zamani wa Dodoma,ambao pia mtasaidiana katika shida na raha.
"Huwa najisikia vibaya sana kuona wachezaji wengi wa zamani wakipata changamoto za matibabu kwa ukosefu wa fedha na kupelekea umauti wao,ninaamini kwa huduma ya bima ya jamii itakuwa imesaidia sana kuwaondolea mzigo mkubwa wanamichezo na mimi nitawalipia wanachama wote 75 wa awali bima ya jamii kwa miaka miwili,”amesema Mavunde.
Akizungumza kwa niaba,Mwenyekiti wa UFAWAZA Dodoma,Ally Kheri amemshukuru Mbunge Mavunde kwa namna alivyowakimbilia na kuwashika mkono tangu kuanzishwa kwa umoja huo na kuahidi kuuboresha umoja huo ili malengo ya uanzishwaji wake yaweze kutimia.