NA GODFREY NNKO
Ushindi wa Arsenal wa bao 1-0 dhidi ya Watford umeipeleka nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, likiwa ni goli la 100 kwa kocha Mikel Arteta akiwa katika dimba la Emirates.
Aidha, mara ya mwisho kwa Watford kuondoka katika dimba la Emirates na alama tatu ni Januari 2017 baada ya kuichapa Arsenal 2-1 katika mchuano wa EPL.
Mechi hii ni ya ya tano kwa Watford kupoteza kutokana na sita zilizopita dhidi ya Arsenal ambao hawajawahi kukamilisha mechi dhidi ya wapinzani wao hao bila kufunga goli.
Kocha Arteta ambaye alikuwa ameanza vibaya msimu huenda hii ikawa faraja kwake kufuatia mwanzo huo huku kijana wake Smile Smith Rowe akiipa alama tatu Arsenal ndani ya dakika ya 57 na likiwa ni bao lake la tatu kwenye mechi tatu mfululizo.
Nahodha wa Arsenal Pierre-Emerick Aubameyang alikosa tuta kufuatia Danny Rose kumfanyia madhambi Alexandre Lacazette, hata hivyo mlinda mlango Ben Foster alifanya kazi ya ziada kuokoa mchomo huo katika mtanange huo wa Novemba 7, 2021.
Kwa msingi huo, ushindi mfululizo kwa kocha Arteta umeibeba timu hiyo mpaka nafasi ya tano kwa alama 20 kwenye msimamo wa EPL wakifanana alama na West Ham United.
Arsenal katika mtanange huu walishuka dimbani wakiwa na kiu ya kuendeleza ubabe uliowapa ushindi wa 2-0 katika mchuano wa awali wa EPL dhidi ya Leicester.
Huku, Watford ya kocha Claudio Ranieri nayo ikipania kuruka kiunzi baada ya kupigwa bao 1-0 na Southampton hivi karibuni.
Arsenal walipoteza nafasi nzuri kwa Watford katika dakika ya 36 baada ya penalti ya nahodha na mshambuliaji Pierre-Emerick Aubameyang kupanguliwa na kipa Ben Foster.
Mkwaju huo ulitokana na tukio la fowadi Alexandre Lacazette kuchezewa visivyo na beki Danny Rose ndani ya kisanduku.
Watford walikamilisha mtanange huo na wachezaji 10 dimbani baada ya kiungo raia wa Slovakia, Juraj Kucka kuonyeshwa kadi ya pili ya njano mwishoni mwa kipindi cha kwanza.
Watford wanaoshikilia nafasi ya 17 wanafana na Aston Villa waliomfuta kazi kocha Dean Smith baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa miaka mitatu sasa.
Kocha Smith mwenye umri wa miaka 50 anaondoka Villa baada ya Southampton kuwatandika 1-0 katika EPL mwishoni mwa wiki katika dimba la St Mary’s na ilikuwa mechi ya tano mfululizo kwa Villa kupoteza msimu huu.
Wakati huo huo, Leicester City imetoshana nguvu na Leeds United ya sare ya bao 1-1 katika mchezo wa Ligi Kuu England uliopigwa Novemba 7, 2021 katika dimba la Elland Road.
Leeds United ambao walikuwa nyumbani wamepata bao kupitia kiungo mshambuliaji Raphinha Belloli dakika ya 26 ya mchezo akimpiku mlinda mlango Kasper Schmeichel.
Hata hivyo, Barnes alisawazisha bao hilo likiwa ni bao la 13 kwake ingawa kabla ya hapo walikosa nafasi nyingi za wazi.
Matokeo hayo yanaifanya Leeds United ya kocha Marcelo Bielsa kushika alama tatu muhimu kutoka kwenye mstari wa kushuka daraja wakati Leicester ya kocha Brendan Rodgers ambaye anahusishwa kujiunga na Manchester United kurithi mikoba ya Ole Gunnar Solskjaer ikishika nafasi ya 12.
Aidha, kocha Antonio Conte alianza kibarua cha kudhibiti mikoba ya Tottenham Hotspur kwenye soka ya EPL kwa kuongoza vijana wake kusajili sare tasa dhidi ya Everton katika dimba la Goodison Park.
Tags
Michezo