NA HADIJA BAGASHA
BANDARI ya Tanga imepokea meli kubwa iliyobeba shehena ya mzigo wa Klinka tani 50,000 malighafi itakayosafirishwa kuelekea nchini Rwanda katika kiwanda cha saruji cha Prime Cement Ltd.
Serikali ya Rwanda imeanza kuitumia Bandari ya Tanga kupitishia shehena
ya mizigo yake ikiwa ni miezi miwili toka ziara ya Balozi wa nchi hiyo
kutembelea Bandari ya Tanga na kuvutiwa na ufanyaji kazi wa bandari
hiyo.
Meli hiyo yenye urefu wa mita zaidi ya 150 na kina cha
mita 12 inayoitwa Star Fighter' Majuro yenye namba za usajili 9642198
kwa mujibu wa Wakala wa Kimataifa wa Bahari (IMO) imetia nanga siku ya
Ijumaa iliyopita ikitokea nchini Saudi Arabia.
Katika kipindi cha
mwezi Novemba katika bandari ya Tanga meli hiyo inakuwa ni ya pili
kushusha shehena kubwa ya mzigo kutokea nchi za Mashariki ya Kati ambayo
ilishusha shehena ya mzigo wa mafuta tani 30,000.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima ameongoza viongozi wa Serikali,
Mamlaka ya Bandari na waandishi wa habari kupokea meli hiyo na kusema
kuwa ujio wa meli hiyo na shehena ya mzigo uliobeba si tu utaongeza
mapato ya serikali kupitia kodi mbalimbali za bandari na TRA,pia itainua
uchumi wa wajasiriamali wadogo wadogo haswa wanaotoa huduma za
vyakula,malazi kutokana takribani malori 200 yanatarajiwa kuja kubeba
mzigo huo,hivyo madereva watahitaji vyakula,maji na malazi.
Amesema
kuwa, ujio wa shehena ya mizigo hiyo ni mafanikio ya uwekezaji mkubwa
wa maboresho ya miundombinu katika Bandari ya Tanga ambao umeweza
kufanywa na Serikali ya awamu ya Sita.
"Meli imekuja na
neema,tutapata mapato ya serikali,wananchi watafanya biashara mbalimbali
za vyakula,malazi na ujio huu ni juhudi za Serikali katika uwekezaji
kwenye bandari hii ambapo zaidi ya shilingi bilioni 480 zimekwa katika
upanuzi na ukarabati,"amesema.
"Pia nimewaomba Prime Cement Ltd kufanya mkutano na wamiliki wa
magari makubwa ya mizigo ya Tanzania kuongea nao ili wabebe shehena hii
badala ya kutumia magari yao tu ambayo ni machache na yatatumia muda
mwingi kumaliza shehena hiyo,"ameongeza Mkuu huyo wa mkoa.
Pia
amesema kuwa, baada ya kukamilisha hili la bandari ya Tanga kinachofuata
sasa ni mradi mwingine mkubwa wa reli ili kuwawezesha wenye mzigo yao
inapofika bandarini basi inakuwa rahisi kusafirisha kwa njia ya treni.
Kwa upande wake,Meneja wa Bandari ya Tanga,Donald Ngaile amasema kuwa ndani ya mwezi huu bandari hiyo tayari imeshahudumia tani 80,000 ya shehena za kichele (clinker) na kimiminika mbali na makontena.
Ngaile amesema kuwa, kutokana na maboresho yanayoendelea Bandari hiyo inatarajia kuongeza shehena ya mizigo kutoka tani laki 750 hadi Milioni 3 kwa mwaka.
Amesema kuwa, kuanza kutiririka kwa shehena ya mizigo ni mwanzo mzuri wa bandari hiyo kuanza kufungua na kuanza kufanya biashara kwa ufanisi kwa Bandari hiyo.
"Hii bandari ina miaka 130 kutokana na msukumo wa Serikali pamoja na mboresho yanayofanyika sasa tutaanza kupokea shehena kubwa ya mizigo katika Bandari yetu,"amesema Ngaile.
Meneja Uendeshaji Biashara wa Prime Cement Ltd, Mvayo Fabrice amesema kuwa, kampuni yake imeamua kutumia bandari hiyo kwa sababu kuu mbili ambazo ni kijografia kwani bandari hiyo ipo karibu sana kuhudumia moja kwa nchi za Afrika Mashariki na pia wameepuka msongamano wa meli katika nchi katika bandari ya Dar es Salaam.
DIRAMAKINI BLOG imeelezwa kuwa, kuja kwa meli hiyo katika bandari ya Tanga imeifanya kuwa na nguvu kubwa ya kuhudumia mizigo ya kimataifa ikiwemo mafuta,gesi,makontena na kemikali za viwandani.
Pia inatumika na meli za visiwa vya Unguja na Pemba kuja kuchukua bidhaa za biashara hasa za vyakula.