NA GODFREY NNKO
MCHEZAJI wa Kimataifa katika Klabu ya Simba ambaye ni raia wa Ghana, Bernard Morrison amesema kuwa, anathamini sana mchango wa Klabu ya Yanga katika maisha yake ya soka nchini Tanzania.
Winga huyo ameyabainisha hayo leo Novemba 23,2021 kupitia ujumbe maalum alioutoa katika ukurasa wake wa Facebook.
Ujumbe huo ambao umeonwa na DIRAMAKINI Blog, Winga Bernard Morrison amesema kuwa;
"Kuna mwanzo na mwisho wa kila kitu, hakuna kinachodumu milele. Sote tumekuwa tukingojea uamuzi huu (kwa wema au ubaya), hatimaye wakati umefika na unamaliza mashaka yote na mvutano.
"Nataka tu kila mtu ajue jinsi ninavyoithamini YANGA kwa nafasi waliyonipa ya kuwawakilisha na kuvaa beji yao, hakuna mtu hapa Tanzania aliyejua wala kujali kuhusu kazi yangu hadi LUC AYMAEL aliponileta kucheza hapa.
"Asante kocha kwa kuniamini na kunifanya kuwa mkuu. Kuna msemo kule GHANA usema kuwa "daktari mbaya aliyekutunza hadi daktari mzuri alipofika lazima athaminiwe".
"Hata kama alikuwa mbaya, alikuweka hai mpaka yule bora aje. Hii ni kusema rasmi kwamba, asante kwa YANGA SC na yeyote aliyenifanya nitabasamu au kunipenda nirudi klabuni kwao, bila kusahau mapenzi niliyoonyeshwa na mashabiki wao,"amesema Bernard Morrison.
Winga huyo wa Kimataifa wa Ghana anayecheza Klabu ya Simba, Bernard Morrison ameyasema hayo siku moja baada ya kushinda kesi yake dhidi ya Yanga SC.
Bernard Morrison anafahamika sana kwa vituko vyake akiwa dimbani.
Kesi iliyokuwa ikisikilizwa na Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS).
Taarifa iliyotolewa na Mahakama hiyo imeeleza kuondoa rufaa iliyowasilishwa na Klabu ya Yanga dhidi ya Mchezaji huyo raia wa Ghana anayecheza nchini Tanzania.
CAS wameeleza kuwa kesi hiyo ilitolewa maamuzi na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka nchini Tanzania (TFF) Agosti 12, 2020. I
Imeelezwa kuwa mkataba wa awali wa Morrison uliisha Julai 14, 2020, Morrison alilazimika kulipa kiasi cha fedha Dola za Marekani (USD 30,000) baada ya kushindwa kusaini mkataba wa pili na Yanga SC.
Yanga SC walipeleka suala hilo CAS wakidai kulipwa kiasi cha Dola za Marekani 200,000 baada ya Mchezaji huyo kuvunja mkataba na Klabu hiyo.
Aidha,Mahakama ya CAS ilikaa Julai 29, 2021 na kutupilia mbali rufaa ya Yanga SC ikidaiwa haina mashiko.